Rais Muhammadu Buhari ametakiwa kuchukua likizo ya matibabu nchini Nigeria
Kundi moja la watu mashuhuri nchini Nigeria limemtaka rais wa taifa hilo Muhammadu Buhari mwenye umri wa miaka 74 kuchukua likizo ya matibabu kufuatia wasiwasi mwingi kuhusu hali yake ya afya.
Hali yake ya afya imekuwa ikidorora kufuatia hatua yake ya kutohudhuria mikutano miwili ya mabaraza ya mawaziri kulingana na kundi hilo.Bwana Buhari alichukua wiki saba za likizo ya matibabu mnamo mwezi Januari na kusafiri hadi nchini Uingereza kwa matibabu.
Wakati aliporudi nyumbani mnamo mwezi Machi alisema kuwa hajawahi kuwa mgonjwa kupita kiasi maishani mwake.
Bwana Buhari hajatangaza anaugua ugonjwa gani, lakini alisema kwamba aliongezewa damu .
Rais huyo hajaonekana hadharani kwa kipindi cha wiki moja sasa, na hatua ya kutohudhuria mkutano wa baraza la mawaziri pamoja na ibada ya kila wiki ya Waislamu inayofanyika siku ya Ijumaa, imesababisha uvumi zaidi kuhusu hali yake ya kiafya, kundi hilo la watu 13 limesema katika taarifa.
Kundi hilo linashirikisha wanaharakati wenye ushawishi mkubwa akiwemo wakili Femi Falana, mchanganuzi wa maswala ya kisiasa Jibrin Ibrahim na kiongozi wa shirika la Transperance International tawi la Nigeria Anwal Musa Rafsanjani.
Raia hao 13 wanasema kuwa walilazimika kumshauri rais Buhari kusikiza ushauri wa daktari wake wa kibinafsi kwa kuchukua mapumziko ili kuangazia afya yake bila kuchelewa.
Wasaidizi wa Buhari hawajatoa tamko lolote kuhusu taarifa hiyo.
Wiki iliopita msemaji wa rais Buhari Garba Shehu alisema kuwa bwana Buhari alikuwa akifanya mambo polepole huku akiendelea kupona kufuatia kipindi kirefu cha matibabu nchini Uingereza.
Comments
Post a Comment