Hayo yameelezwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa hesabu za serikali (CAG) Charles Edward Kichere, alipokuwa akitoa taarifa kwa mwaka wa fedha 2019/2020 kwa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan katika Ikulu ya Chamwino, jijini Dodoma.
Ameeleza kuwa kuna changamoto mbalimbali ambazo ameshauri serikali iziangalie, ili shirika hilo liweze kutekeleza majukumu yake.
Katika Ripoti ya Mkaguzi ameeleza ubadhirifu mkubwa uliofanywa katika shirika la bandari.
Baada ya kukabidhiwa ripoti hizo, Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa katika shirika la bandari kuna ubadhirifu wa karibu shilingi bilioni nne za Kitanzania, hivyo amemsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Bandari, Mhandisi Deusdedit Kakoko ili kupisha uchuguzi.
''Nimeona ubadhirifu mkubwa uliofaywa katika shirika la bandari, ninaomba TAKUKURU hii ni kazi maalum jishughulishe pale, ninajua Waziri Mkuu aliunda kamati na wakafanya uchunguzi kidogo pale na mambo yaliyotoka, hatua chache zilichukuliwa,
''lakini imani yangu ni kwamba kama kuna ubadhirifu ndani ya shirika, na kwa ripoti ile ulionikabidhi jana jioni kuna ubadhirifu kama wa sh bilioni 3.6 karibu bilioni nne lakini wakati Waziri Mkuu alipofanya uchunguzi waliosimamishwa ni wa chini.Naomba mara moja kutoa agizo la kumsimamisha Mkurugenzi Mkuu wa bandari , halafu uchunguzi uendelee''. Amesema Rais Samia
CAG Kichere amekabidhi ripoti 21 kwa Rais Samia, zikigusa maeneo mbalimbali baadhi ni kama vile ripoti ya ukaguzi wa serikali kuu ,Mashirika ya Umma, Mamlaka za serikali ya mitaa, miradi ya maendeleo na TEHAMA.
Rais Samia Suluhu Hassan ametoa agizo kwa CAG kupitia fedha zote zilizotoka kuanzia mwezi Januari mpaka mwezi Machi zilizokwenda kwenye utekelezaji wa miradhi ya maendeleo zionekane.
Pia amemtaka CAG kutopata utata katika kusema mapungufu wakati anapotekeleza wajibu wake.
''Naomba sana ulimi wako usiwe na utata kama kuna shirika halifanyi vizuri, tuambie hili halifanyi vizuri, kama bodi haisimami vizuri tuambie bodi hii haisimami vizuri kwa sababu tutakaposema mapungufu ndipo tutakapoweza kurekebisha na tukaweza kufanya vizuri zaidi, tukinyamaziana kwa kutazamana sura hatutarekebisha na tutawaumiza wananchi naomba sana ripoti yako iwe wazi zaidi, utakaponiletea ukaguzi wa mashirika uwe wazi zaidi ili tujue tunachukua hatua gani''. Amesema Rais Samia.
Comments
Post a Comment