UGANDA:Mwendesha bodaboda ajichoma moto baada ya kukataa kutoa rushwa

Hussein Walugembe
TWAHA KAWEESA
Kijana mwenye umri wa miaka 29-ambaye ni mwendesha bodaboda nchini Uganda amefariki baada ya kujichoma moto mwenyewe katika kituo cha polisi.

Kwa mujibu wa walioshuhudia kisa hicho mjini Masaka, Kusini mwa Uganda, bwana huyo aliamua kujiua baada ya polisi kutaka awape rushwa ili wamrudishie pikipiki yake walioikamata kwa madai kuwa alivunja sheria za kutotoka nje usiku.

Mwandishi wa BBC, Issaac Mumena anasema mwendeshaji huyo wa boda boda anayefahamika kwa jina Hussein Waugembe alijichoma mwenyewe moto baada ya kushindwa kuafikiana na askari wa usalama barabarani wa wilaya ya Masaka, ambao walikataa kumpatia pikipiki yake.

Marehemu alikwenda kudai bodaboda yake iliyokamatwa kwa kuvunja amri ya kutoka nje katika kituo cha polisi Masaka, marehemu alimuomba mkuu wa kituo cha polisi kumpatia pikipiki yake lakini hawakumpatia.

Kwa mujibu wa shuhuda wa tukio hilo marehemu alikwenda kwenye ofisi ya polisi ya usalama barabarani na kukutana na askari polisi aliyechukua pikipiki yake na kumueleza kwamba amechoshwa kuzungushwa .

Kijana huyo alipofika kituoni alimwambia wa askari wa polisi wa usalama barabarani ampe bodaboda yake ndipo askari alipochukua simu yake na kuanza kumpiga picha kijana huyo,

Ndipo kijana huyo alipochukua mafuta ya petroli na kujimwagia mwilini, na baadaye akatoa njiti za kiberiti na kumwambia polisi ampatie pikipiki yake, polisi hakumujibu hivyo marehemu akajiwasha moto na kumfuata polisi lakini polisi aliweza kukimbia na hivyo kijana huyo kuteketea moto.

Habari hizo zilisambaa kwa haraka na mara moja na waendesha bodaboda wakazingira kituo cha polisi Masaka.
boda

Waendesha boda boda wamelaani vikali vikosi vya usalama barabarani tangu zuio la bodaboda kutobeba abiria na kusema hii imekuwa tabia ya polisi kuwanyanyasa wakati huu kwani mwenzao alifuatilia pikipiki yake tangu siku ya Jumatatu huku wakimtaka awape kitu kidogo, alielezea mwendesha boda boda:

"Wao lengo lao ni pesa tu, kila wakati wanakuomba pesa, kama ukiwa na pesa unapewa kama hauna pesa huwezi kupewa, hicho ndicho kilichomufikisha Hussein kujichoma moto katika ofisi ya polisi ni kutokana na manyanyaso ya polisi," shuhuda alieleza.

Msemaji wa Jeshi la polisi Fred Enanaga amevieleza vyombo vya habari kwamba tayari askari wawili wamekamatwa kutokana na tuhuma za rushwa na uzembe.

Mpaka sasa maafisa wawili wamekamatwa , na hawa wawili ndio waliokuwa wanaweka msukumo kwa marehemu kuwapatia rushwa ili kumpatia pikipiki yake akiwemo Sajeti Juliu pamoja na Sajeti Ibrahim Ssesanga mkuu wa kituo wa usalama barabarani.

"Hawa walifanya kazi kwa uzembe mkubwa kukatalia pikpiki bila kutoa sababu yoyote,". Msemaji wa Polisi.

Hili sio tukio la kwanza la Bodaboda tangu kuzuiwa kubeba abiria mwezi jana tarehe 29, Jeshi la Mgambo lilimpiga mwanaume mmoja na kufariki wilayani Ayamu kaskazini mwa Uganda, na tarehe 24 mwezi huo wa Juni askari wa jeshi la UPDF alimupiga risasi mwendesha Boda Boda na kufariki.

Tangu rais Yoweri Museveni, alipopiga marufuku ya pikipiki za boda boda kubeba abiria kwa kuzuia kuenea kwa maambukizi ya virusi vya covid19 mwezi machi, boda boda wamekuwa na wakati mgumu na kutishia kufanya maandano mapema mwezi huu lakini yalizimwa na jeshi la polisi.

Comments