Seif Sharif Hamad aliwahi kuwa Mwalimu wa shule kabla ya kuacha chaki na kuzama katika siasa.
Jina lake si geni kwa wafuatiliaji wa siasa za Tanzania. Yupo katika ulingo huo tangu akiwa Chama cha Mapinduzi (CCM), kabla ya kuwepo Chama cha Wananchi (CUF) na sasa ACT Wazalendo.
Siku ya Jumapili, bwana Hamad, ama maarufu zaidi kama Maalim Seif, alichukua fomu za kugombea urais wa Zanzibar mwezi Oktoba. Hii itakuwa mara ya sita kwa Maalim kugombea, akishindwa katika mara tano zilizopita.
Wakati uchaguzi wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi unafanyika Tanzania nzima mwaka 1995. Mwanasiasa huyomwenye umri wa miaka 76 kwa sasa, alikiongoza chama cha CUF kwa upande wa Zanzibar katika mbio za Urais.
Baada ya kushindwa kukitwaa kiti hicho, miaka mitano baadaye 2000 alijaribu tena na hakufanikiwa vile vile. Matokeo ya uchaguzi huu yalisababisha ghasia za kisiasa Januari 2001.
Mkasa wa mauaji ya 2001 ulihusisha wanachama wa CUF walioamua kuandamana kwa amani kupinga matokeo ya uchaguzi, wakiamini chama chao kimeporwa ushindi, kwa upande mwengine vikosi vya usalama vikiongozwa na Jeshi la Polisi viliyazima maandamano hayo kwa risasi za moto.
Kwa mujibu wa ripoti ya Human Rights Watch (HRW) iliyopewa jina, "Tanzania: Risasi zilinyesha kama mvua", inakisia watu 35 waliuwawa, wapatao mia sita walijeruhiwa na takribani 2000 walikimbilia nchi jirani.
Miaka minne baada ya mauaji hayo Maalim alijitosa tena katika kinyang'anyiro cha urais mwaka 2005, akichuana na Amani Abeid Karume, mtoto wa Rais wa kwanza wa Zanzibar Sheikh Abeid Karume. Amani aliyekuwa akiwania muhula wake wa pili na wa mwisho alimbwaga tena Maalim katika mbio za Urais.
Mauaji ya 2001 na mchafukoge wa kisiasa uliofuatia ulichangia kuwaleta pamoja Rais Amani na Katibu Mkuu wa CUF kwa wakati huo Maalim Seif katika meza ya mazungumzo iliyopelekea kuasisiwa serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Tarehe 31/07/2010, Wazanzibari kupitia kura ya maoni walichagua kwa zaidi ya asilimia 60 kuongozwa kwa mfumo wa serikali hiyo ambayo kwa mara ya kwanza iliundwa baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2010 na kuongozwa na Dkt. Ali Mohammed Shein huku Maalim Seif akiwa Makamu wa kwanza wa Rais.
Uchaguzi wa 2010, uliomuweka madarakani Rais anayemaliza muda wake sasa haukushuhudiwa vurugu lolote huku Maalim akigaragazwa tena. Mwanasiasa huyo alishukuru kwa uchaguzi usiokuwa na vurugu pia akampongeza Dkt Shein kwa ushindi, kisha alitoa kauli iliyotuliza wafuasi wake kwa kusema, "hakuna mshindi wala mshindwa, washindi ni Wazanzibari wote".
Kwa mara ya kwanza katika historia ya siasa za visiwa hivyo, siasa yenye taharuki, uhasama na hata fujo wakati wa uchaguzi, wanachama wa CCM na CUF walipeperusha bendera za vyama vyao kwa pamoja kusherehekea ushindi huo.
Vuta n'kuvute ya kisiasa ilirudi tena Zanzibar katika uchaguzi wa Oktoba 2015 baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kuyafuta matokeo ya uchaguzi na kuitisha uchaguzi mwengine.
Chama kikuu cha upinzani CUF kilisusia uchaguzi wa marudio, huku kikidai kuwa kilipata ushindi katika uchaguzi wa awali. Tangu wakati huo hadi sasa wakati imebaki miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu, yale maridhiano ya kisiasa yaliyoleta ahueni na kupunguza siaza chafu za uhasama na ubaguzi yanalegalega.
Mustakbali wake kisiasa ni upi?
Siku chache zilizopita mkongwe huyo wa siasa alitangaza kuingia tena katika kinyang'anyiro cha kugombea Urais wa Zanzibar kupitia ACT Wazalendo, kisha alichukua fomu rasmi.Kwa hesabu zisizo na shaka, hiyo itakuwa ni mara yake ya sita lakini ni ya kwanza kupitia chama hicho kilichopata usajili wake kamili Mei 2014.
Jambo lisilo hojika wala kukatalika juu ya Maalim ni kuhusu ushawishi wake. Bado ana ushawishi mkubwa kisiasa katika visiwa hivyo. Hata wakati anaondoka CUF na kwenda ACT palizuka msemo kutoka kwa wafuasi wake wakisema, "ulipo tupo".
Msemo huo haukuwa na uzito wa kimatamshi tu, pia ulikuwa na uzito wa kivitendo, kwani wafuasi wengi wa CUF walianza kuhama na wanaendelea kuhama hadi sasa kumfuata Maalim katika chama chake kipya.
Licha ya ushawishi alionao katika visiwa hivyo vyenye wakaazi takribani milioni moja laki tatu na ushei, lipo linahojika kuhusu yeye. Je, ataendelea kuwa na ushawishi na mvuto huo wa kisiasa hata ikiwa atabwagwa kwa mara ya sita?
Mchambuzi wa siasa na mwandishi mkongwe wa habari aliyeripoti chaguzi za Zanzibar kuanzia ule wa 2000, 2005 na 2010, Mohammed Abdulrahman anajibu swali hilo kwa kusema, "mustakbali wa kisiasa wa Maalim utategemea matokeo ya uchaguzi wa mwaka huu. Iwapo atashindwa kihalali au kimizengwe, mvuto wa kisiasa alionao sasa utaondoka".
Wakati Maalim anatangaza nia ya kugombea Urais alikiri uwepo wa sauti alizoziita chache zilizomtaka apumzike na kijiti hicho amwachie mtu mwegine.
Kwa kutumia utabiri wa kisiasa kuna kila sababu ya kuamini, ikiwa hatofanikiwa mara hii sauti hizo zitaanza kusikika wazi wazi na kwa wingi wa idadi. Na huenda huo ndio ukawa mwanzo wa mwisho wake kisiasa.
Bilashaka kitu pekee kitakacho mnusuru kubakia na mvuto alionao kwa wafuasi wake ni ushindi katika uchaguzi huu. Mwenyewe daima huamini anashinda katika chaguzi zote zilizopita, lakini hulalamika kuporwa ushindi, hadithi yake ni hiyo hiyo kila baada ya miaka mitano. Hadithi ambayo imenza kuchokwa.
Swali ni; Je, hadithi yake ya mara hii itabadilika kwa wafuasi wake au itabaki kuwa ile ile? Hilo ni la kusubiri na kuona.
Historia yake
Seif Sharif Hamad alizaliwa Mtambwe, kisiwani Pemba, Zanzibar, Oktoba 1943. Alisoma elimu yake ya msingi na upili katika visiwa hivyo kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kusomea shahada ya kwanza ya Sayansi ya Siasa.
Huyu ni mwanasiasa aliyehudumu katika nyadhifa mbalimbali ndani ya serikali ya mapinduzi tangu akiwa CCM hadi CUF.
Kabla ya kuwa mwanasiasa alikuwa Mwalimu aliyesomesha shule kadhaa Unguja na Pemba.
Kuna kila dalili ya kuwa safari yake ya kisiasa itahitimika akiwa katika chama chake kipya.
Kitendawili kilichobaki ni ikiwa itahitimika kwa kufanikiwa zile ndoto za muda mrefu za kuwa Rais ama itahitimika kwa kuwa simba wa kisiasa aliyepambana na hatimae akamalizika bila lengo kuu kutimia.
Muda utazungumza!
*Chanzo cha picha ACT WAZALENDO
Comments
Post a Comment