Jumapili ya Tarehe 25 Oktoba, mamilioni ya Watanzania watapiga kura kuchagua viongozi watakaowaongoza kwa miaka mitano ijayo. Huu utakuwa uchaguzi wa sita toka nchi hiyo iliporejea kwenye siasa ya mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.
Kama ilivyo kwa chaguzi zote duniani kuna mambo ya msingi ambayo hutoa taswira ya mchakato mzima utakavyokuwa, na kwa upande wa Tanzania kuna mambo matano ambayo ni ya muhimu kuyafahamu.
Short presentational grey line
Magufuli vs Lissu ama Magufuli vs Membe?
Toka uchaguzi wa kwanza wa mwaka 1995, mbio za uchaguzi nchini Tanzania huongozwa na vinara wa kinyang'anyiro cha urais.
Mvuto na ushawishi wa wagombea wa chama tawala cha CCM na upinzani huwa ndiyo jambo linalotawala zaidi katika vinywa vya wapiga kura zaidi ya sera na ilani zao.
Mwaka 1995, kinyang'anyiro kilikuwa baina ya Benjamin Mkapa wa CCM na Augustino Mrema wa NCCR-Mageuzi, na licha ya kupokea upinzani mkali Mkapa aliibuka na ushindi kwa 61% ya kura. Mwaka 2000, Mkapa aligombea muhula wa pili na kwa wakati huo mpinzani mkuu alikuwa Prof Ibrahim Lipumba wa CUF. Hata hivyo nguvu ya upinzani iliporomoka na Mkapa akaibuka na ushindi wa 71%.
Uchaguzi wa mwaka 2005 CCM ilimsimamisha Jakaya Kikwete ambaye alikuwa na ushawishi mkubwa na kuzoa 80% ya kura, Prof Lipumba alimfuatia kwa mbali akipata 10% ya kura. Mwaka 2010 Kikwete aligombea kwa muhula wa pili dhidi ya Dkt Wilboad Slaa wa Chadema. Ushawishi wa upinzani ulipanda, japo Kikwete alirudi madarakani lakini alishinda kwa 62% ya kura.
Miaka mitano iliyopita CCM ilimsimamisha John Magufuli, huku upinzani ukimsimamisha Edward Lowassa. Ulikuwa mchuano mkali kweli kweli na kwa mara ya kwanza toka siasa za vyama vingi kurejea Tanzania, mgombea wa CCM hakufikisha 60% ya kura. Magufuli alipata 58% ya kura huku Lowassa akipata 39%.
Tundu Lissu ametangaza nia ya kuchuana na Magufuli Oktoba
Mwaka huu 2020, Magufuli ndiye mgombea pekee aliyechukua fomu ya kugombea urais kupitia CCM, hivyo ni dhahiri kuwa atapambana kurejea kwa muhula wa pili na wa mwisho madarakani kwa mujibu wa katiba. Kete yake kubwa katika uchaguzi ujao utakuwa rekodi yake ya kuleta mabadiliko na maendeleo ya kasi katika sekta muhimu za uchumi kama, ujenzi, uchukuzi na afya.
Kwa upande wa upinzani mpaka sasa, bado haijakuwa wazi ni nani atakuwa kinara wao. Kwa upande wa chama kikuu cha upinzani Chadema, aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu anaongoza mbio za kupewa ridhaa na chama chake. Lissu amekuwa ni moja ya wakosoaji wakubwa wa serikali ya Magufuli, mwaka 2017 alishambuliwa vibaya kwa risasi, na kulazimika kupelekwa ughaibuni kwa matibabu.
Mpaka sasa bado yungali ughaibuni, na hata fomu ya kugombea urais ndani ya chama amechukuliwa na mwakilishi. Mara kadhaa amekuwa akiahirisha kurejea Tanzania akitaja sababu za kiusalama. Kwa sasa ameahidi kurejea mwisho wa mwezi huu. Nguvu ya Lissu ipo katika ujenzi wake wa hoja, na uwezo wake wa kumkabili Magufuli.
Mwanansiasa mwengine ambaye anatarajiwa kugombea kwa tiketi ya upinzani ni Bernard Membe. Membe amehudumu kama Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania wakati wa Kikwete na alikuwa ni moja ya mawaziri wenye nguvu na ushawishi mkubwa. Hata hivyo, toka alipoingia madarakani Magufuli, alikuwa akitajwa kuwa anamhujumu kwa kupanga kuchuana naye ndani ya chama mwaka huu. Mwanasiasa huyo alifukuzwa uanachama wa CCM na wiki hii amerejesha kadi ya uanachama.
Japo bado hajajiunga rasmi na upinzani, duru za kisisasa zinaonesha kuwa kuna harakati zinaendelea baina yake na chama cha ACT-Wazalendo. Wiki ilopita, Membe aliiambia BBC kuwa atagombea urais endapo upinzani utaungana na kumuomba agombee kwa mwamvuli wao.
Je, upinzani utaungana?
Mafanikio makubwa ya upinzani miaka mitano ilopita yalitokana na vyama vikuu kuunganisha nguvu kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) na kusimamisha mgombea mmoja Edward Lowassa ambaye pia alikuwa na ushawishi.
Vyama vinne vya Chadema, CUF, NCCR na NLD viliunda umoja huo, lakini hii leo muungano huo haupo tena.
Hata hivyo, sura ya upinzani pia imebadilika, ACT-Wazalendo kilikuwa chama kidogo mwaka 2015 kwa kuambulia mbunge mmoja tu, lakini sasa kimeongeza ushawishi wake.
ACT imepokea mtaji mkubwa wa kisiasa baada ya mgogoro wa kiuongozi ndani ya CUF baina ya Mwenyekiti Prof Lipumba na aliyekuwa Katibu mkuu Maalim Seif Shariff Hamad. Mwisho wa mgogoro huo Maalim Seif na wafuasi wake walilazimika kuhamia ACT. Na sasa chama hicho kinatazamiwa kuvuna ushawishi wa Maalim Seif katika siasa za Zanzibar kupata kura na uwakilishi mkubwa zaidi.
ACT imekiandikia rasmi Chadema kutaka kushirikiana nacho katika uchaguzi ujao, hata hivyo mpaka sasa bado haijakuwa wazi endapo vyama hivyo vitaunganisha nguvu.
Jibu la swali la nani ataminyana na Magufuli baina ya Lissu na Membe pia litategemea na uwepo wa umoja wa upinzani. Hata hivyo, endapo wapinzani hawatakuwa wamoja ifikapo Oktoba, ni dhahiri kuwa Magufuli na CCM watapata mafanikio makubwa.
Chaguzi mbili ndani ya moja
Tanzania kuna serikali mbili ya Muungano na ya Zanzibar, na hivyo mamlaka za uchaguzi pia zinachukua sura hiyo. Kuna uchaguzi wa Muungano ambao unahusisha Watanzania wa Bara na Zanzibar na unasimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Pia kuna uchaguzi wa Zanzibar unaosimamiwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).
Katika uchaguzi wa Muungano wapiga kura wanachagua nafasi tatu, Rais, Mbunge na Diwani na kwa upande wa Zanzibar kura mbili huongezeka, Rais wa Zanzibar na Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi.
Tume hizo mbili NEC na ZEC zina mamlaka kamili katika chaguzi zinazosimamia na haziingiliani katika maamuzi. Mwaka 2015, aliyekuwa mwenyekiti wa ZEC Jecha Salum Jecha alitangaza kufuta matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar lakini matokeo ya ubunge na urais wa muungano kwa upande wa Zanzibar haukuathiriwa na maamuzi hayo ya ZEC.
Hata hivyo, vyama vinavyoshiriki katika chaguzi hizo lazima viwe na uwakilishi pande zote mbili za muungano, na husajiliwa chini ya ofisi ya msajili ambayo kimfumo ipo chini ya Serikali ya Muungano.
Upinzani mkali Zanzibar
Toka uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi wa mwaka 1995, visiwani Zanzibar kumeshuhudiwa upinzani mkali wa kisiasa ikilinganishwa na uchaguzi wa Muungano (ama upande wa Bara).
Upinzani mkali umekuwa baina ya chama tawala CCM na upinzani CUF chini ya Maalim Seif. Na kwa kuwa mwaka huu Maalim yupo upande wa ACT na anatarajiwa kugombea urais kwa mara ya sita.
Uchaguzi wa kwanza 1995 ulishuhudia Salmin Amour wa CCM akipata ushindi mwembamba wa 50.24% huku Maalim Seif akipata 49.76%. Mwaka 2000 CCM ilimsimamisha Amani Abeid Karume ambaye alishinda kwa 67.04% ya kura huku Maalim 32.96%. Mwaka 2005 Karume alishinda awamu ya pili kwa 53.2% Maalim akipata 46.1%. 2010 CCM ilimsimamisha Dkt Shein na kupata ushindi wa 50.11% huku Maalim wa CUF akipata 49.14%.
Maalim Seif anatarajiwa kugombea urais wa Zanzibar kwa mara ya sita mfululizo.
Mwaka 2015 matokeo ya uchaguzi yalifutwa, na uchaguzi kurudiwa 2016 japo chama kikuu cha upinzani CUF kilisusia kushiriki. Dkt Shein alishinda kwa kishindo kwa kupata 91% ya kura.
Chaguzi zote za Zanzibar kasoro mwaka 2010 zimeshuhudia malalamiko ya wizi wa kura na udanganyifu, uvunjifu wa haki za binaadamu na ghasia.
Mwaka 2010 hali ilikuwa tulivu kutokana na kura ya mabadiliko ya katiba ya kuwezesha kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Baada ya uchaguzi wa 2010, Maalim Seif alichukua nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na CUF kuunda sehemu ya mawaziri wa baraza la mapinduzi. Hata hivyo ushirikiano wao haukufanikiwa kama vile ilivyotarajiwa awali na mwishowe haukuwezesha hali ya uchaguzi kuendelea kuwa tulivu mwaka 2015.
Mwishoni mwa wiki CCM inatarajiwa kuchaguwa mgombea wake wa uchaguzi mwaka huu na ushindani mkali unatarajiwa kuendelea kutolewa na Maalim na chama chake kipya.
Idadi ya wapigakura yaendelea kuongezeka
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) bado ingali inafanya maboresho ya daftari la wapiga kura, lakini takwimu za wali zilizotolewa na tume hiyo mwezi Machi zinaonesha kuwa wapigakura nchini humo wamefikia takribani 30,187,987. Idadi rasmi inatarajiwa kutolewa na tume hiyo hivi karibuni.
Miaka mitano iliopita jumla ya idadi ya wapigakura 23,161,440, japo ni asilimia 67.34 ndio walipiga kura (sawa na watu 15,596,110). Idadi ya wapiga kura imekuwa ikiongezeka kwa kasi kila mwaka wa uchaguzi nchini Tanzania ambapo mwaka 1995 waliandikishwa wapigakura 8,929,969 na idadi ilipanda mpaka kufika 20,137,303 mwaka 2010.
Comments
Post a Comment