TARURA YAWAJENGEA DARAJA WANANCHI WILAYANI MVOMERO


Muonekano wa ujenzi wa Daraja la Mto Mjonga (suspension foot bridge), liliopo Wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro, linalojengwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), likiwa limefikia asilimia 80 kukamilika, daraja hili ni kiunganishi cha Vijiji vya Digoma na Digalama.

……………………………………………………………………

Wakazi wa Kijiji cha Digoma, kata ya Diongoya Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro wameipongeza Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kujenga daraja la kudumu katika mto Mjonga litakalounganisha Kijiji hicho na maeneo mengine ya Wilaya ya Mvomero.

Wakizungumza katika mahojiano maalum wakazi hao wameipongeza TARURA kwa kujenga daraja hilo litakalotumiwa na watembea kwa miguu pia litapitisha na baadhi ya vyombo vya usafiri kama pikipiki na bajaji.

“Kivuko kikikamilika kitatuondolea kero ya muda mrefu kwani maji yanapojaa tunapata shida sana kupata huduma za kijamii hivyo kukamilika kwa daraja hili kutapunguza kero zetu za muda mrefu”, alisema Leonard Michael Mkazi wa Kata ya Diongoya.                                                                         

Wakazi hao wamesema kuwa kwa sasa wanatumia shilingi 1000 hadi 2000 kuvuka kwenda upande mwingine kwa kutumia mtumbwi, hivyo kukamilika kwa daraja hilo kutawasaidia sana katika usafirishaji wa mazao yao kwenda sokoni.

Naye, Mtendaji wa Kijiji cha Digoma, Ndg. Omari Nyilika alisema kuwa Daraja la Mto Mjonga ni kiunganishi cha Vijiji vya Digoma na Digalama, hivyo ukamilikaji wa daraja hilo utawasaidia wakazi hao katika shughuli zao za kijamii na kuboresha uchumi wao kwani wanategemea zao la Hiliki pamoja na Kokoa.

“Tunaishukuru sana TARURA kwa kutujengea daraja hili kwani Kijiji chetu hakikuwa na mawasiliano kwa muda mrefu kiasi kilichopelekea wananchi kupata shida kuvuka kwenda upande wa pili kufanya shughuli zao za kimaendeleo, lakini kwa jitihada za TARURA kivuko cha kudumu kimejengwa ili   kutatua kero hiyo ya muda mrefu’’, alisema Mtendaji huyo.

Naye, Meneja wa TARURA Halmashauri Wilaya ya Mvomero, Mhandisi William Lameck alisema ujenzi wa Daraja hilo umekuja baada ya mawasiliano kukatika hasa kipindi cha masika na kusababisha shughuli za maendeleo kukwama na kushindwa kufanya kazi zao kwa kuwa wakazi wa Kata ya Diongoya uchumi wao mkubwa unategemea mazao ya kokoa pamoja na hiliki ili kujipatia kipato.

Ujenzi wa daraja la Mto Mjonga lenye urefu wa mita 42 umefikia asilimia 80 kukamilika na utagharimu shilingi milioni 68.1, ambapo kukamilika kwake kutawezesha wananchi kuvuka kutoka upande mmoja kwenda mwingine ikiwa ni pamoja na kufikisha mazao yao sokoni kwa urahisi.

Comments