WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni Mstaafu George Mkuchika, kwa mamlaka aliyokasimiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa sheria, amefanya uteuzi wa Makatibu Tawala wa wilaya sita.
Katika uteuzi huo Hassan Ngoma ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Singida kuchukua nafasi ya Wilson Shimo ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita.
Kamana Simba ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa wilaya ya Longido mkoani Arusha kuchukua nafasi ya Toba Nguvila ambaye ameteuliwa kuwa mkuu wa wilaya ya Handeni mkoani Tanga.
Naye Faraja Msigwa ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa wilaya ya Karatu mkoani Arusha kuchukua nafasi ya Abbas Kayanda ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa wilaya ya Karatu.
Bahati Joram ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa wilaya ya Malinyi, mkoani Morogoro kuchukua nafasi ya Lameck Lusesa, huku Salum Mtelela akiteuliwa kuwa Katibu Tawala wa wilaya ya Bunda mkoani Mara kuchuku nafasi ya Jonas Nyehoja aliyestaafu.
Uteuzi mwingine ni wa Augustino Chazua ambaye anakuwa Katibu Tawala wa wilaya ya Gairo mkoani Morogoro na anachukua nafasi ya Robert Selasela.
Wateule wote wanatakiwa kuripoti Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dodoma Jumatano keshokutwa saa nne asubuhi.
Comments
Post a Comment