Je siasa za Tanzania zinajifunza nini kutoka kwa ushindi wa Upinzani Malawi ?

Mwanga wa siasa ya Lazarus Chakwera ulifufuliwa baada ya mahakama kufuta matokeo ya uchaguzi wa urais wa mwaka jana
Mwanga wa siasa ya Lazarus Chakwera ulifufuliwa baada ya mahakama kufuta matokeo ya uchaguzi wa urais wa mwaka jana

Rais mpya wa Malawi Dr Lazaraus Chakwera amesimikwa rasmi kushikilia madaraka ya nchi hiyo jirani na Tanzania wiki iliyopita.

Mchungaji Chakwera ameingia madarakani baada ya ushindi katika uchaguzi mkuu uliofanyika nchini humo mwishoni mwa mwezi Juni ambapo vyama vya upinzani nchino humo viliungana katika umoja waliouita Tonse Alliance, vikapambana na chama tawala Democratic Progressive Party (DPP) na kufanikiwa kuking'oa madarakani.

Mwenendo mzima wa uchaguzi ulivyokuwa umetajwa kama ni wa kihistoria, si tu kwa Malawi lakini kwa bara zima la Afrika.

Kiufupi, japo ni mara ya pili kwa mahakama za juu ya nchi kufuta matokeo ya uchaguzi na kuamuru marudio ya uchaguzi - mara ya kwanza ilitokea Kenya - mafanikio ya upinzani nchini humo kuking'oa chama tawala hayajawahi kutokea barani kote Afrika.

Na sasa wafuatiliaji wa maswala ya kisiasa na wachambuzi wanasema yapo mengi ya kujifunza kutoka uchaguzi huo.

Unaweza kusema pia kwamba kilichotokea Malawi ni ukumbusho tu, kwasababu yale yanayosemekana kusaidia kufanikisha ushindi wa upinzani yanajulikana.

Kwamba haitoshi tu kuwa na mgombea mmoja maarufu kuwakilisha chama au muungano wa vyama vya siasa kufikia ushindi kama walioupata muungano wa vyama vya upinzani nchini Malawi.

Magufuli aidhinishwa rasmi na CCM kuwania tena urais
Nini mustakabali wa upinzani baada ya 'kifo' cha UKAWA?
Je, huu ni mwisho wa kisiasa wa Membe?
Kwamba ni mageuzi ya kimfumo na taasisi nyeti ambazo zinawezesha uendeshwaji si tu wa uchaguzi unaofanyika siku moja lakini mchakato mzima wa demokrasia nchini.

Mambo yote haya upinzani nchini Tanzania na barani kote Afrika wanayajua. Wanayazungumzia kila uchao. Labda lililo jipya kutoka Malawi ni ule udhubutu wa kuacha tu kuyazungumzia na kuanza kuyafanyia kazi kabisa.

Katika makala yake ya tarehe 18 Juni 2020 katika gazeti la mtandaoni la Daily Maverick la Afrika Kusini, kiongozi wa upinzani kutoka chama cha ACT Wazalendo Malaam Seif Sharif Hamad aliainisha mageuzi yanayopaswa kufanyika kwa uchaguzi ujao kuwa huru na wa haki
Rais mteule Lazarus Chakwera akipiga kura
Tume huru za uchaguzi wa Zanzibar na taifa, urekebishwaji katika mchakato wa uandikishwaji wapiga kura, mapitio mapya ya mipaka ya majimbo, waangalizi wa kimataifa nk.

Ameendelea kutaja mahakama huru, utendaji wa haki wa jeshi la polisi na usawa na haki katika taarifa za vyombo vya habari vya umma - TBC, ZBC, Daily News, Habari Leo na Zanzibar Leo

Utaona kwamba sehemu kubwa ya orodha ya Maalim Seif imejikita zaidi katika michakato na mienendo ya taasisi mbali mbali, badala ya mageuzi ya taasisi yanayotakiwa kutokea. Inawezekana kwasababu shabaha yake ilikuwa kwa uchaguzi mkuu ulio ndani ya miezi mitatu ijayo.

Maalim Seif na wafuasi wake wamehamia ACT mwaka huu na kukifanya chama hicho kupata makali zaidi
Maalim Seif na wafuasi wake wamehamia ACT mwaka huu na kukifanya chama hicho kupata makali zaidi

Ni mageuzi haya ya kimfumo ambayo yatazifanya taasisi za msingi na michakato yake ifanikishe uchaguzi huru na wa haki.

Katika makala yao katika jarida la mtandaoni la 'From Poverty to Power', Profesa Nic Cheesman mbobezi wa masuala ya demokrasia na maendeleo ya chuo kikuu cha Birmingham na mwandishi wa habari wa Malawi Golden Matonga nguvu ya umma ni ya muhimu katika kuimarisha uhuru na ufanisi wa taasisi za demokrasia

Kwa maneno mengi, kazi ya kuimarisha taasisi hizi si ya kuombwa kutoka kwa watawala, badala yake inatoka kwenye nguvu ya umma. Nafasi ya nguvu ya umma itaonekana huko baadae tena.

Wanaendelea kusema kwamba umoja wa vyama vya upinzani nchini humo ulikuwa msingi muhimu wa kuunganisha kura na kupata asilimia iliyotakiwa kukishinda chama tawala madarakani
Rais Magufuli wa Tanzania
Cheeseman na Matonga wanaongeza kwamba tume huru ya uchaguzi ilichangia pakubwa kwa matokeo yaliyopatikana, na hasa pale palipobadilishwa mwenyekiti aliyesimamia uchaguzi uliopita na kuwepo kwa mwenyekiti mpya

"Inawezekana uchaguzi usingefanyika kabisa kama Tume ya Uchaguzi ya Malawi (MEC) isingepata mwenyekiti mpya Chifundo Kachale. Mwenyekiti Kachale alifanya kazi nzuri ya kupenya katikati ya vigingi vya siasa na vya uendeshaji wa uchaguzi, hata kama alishika wadhifa huo wiki mbili tu kabla ya uchaguzi," wanasema Cheeseman na Matonga

Mchango wa mahakama huru pia umeonekana wazi kwa kilichotokea Malawi. Kwa ujasiri Mahakama ya Katiba na Mahakama Kuu zikaufuta uchaguzi wa awali ambao waliuona kuwa haukuwa wa haki.

Wakaenda mbali na kusisitiza kwamba matakwa ya katiba lazima yaheshimiwe. Kwamba utakapofanyika uchaguzi wa marudio, mshindi lazima apatikane kwa uwiano wa 50%+1, kama ambavyo katiba inataka.

Uwiano huo ulikuwa wa wazi katika katiba kwa muda mrefu, lakini bunge na taasisi zingine zinazoshughulika na uchaguzi ziliupiga danadana na kuukwepesha hata ukapuuzwa na kutokuzingatiwa katika chaguzi zilizopita. Mahakama ikasimama katika nafasi yake, ikasisitiza kwamba katiba lazima itekelezwe.

Cheeseman na Matonga wanaonyesha pia namna Rais Peter Mutharika alivyojaribu kutaka kuviweka vyombo vya ulinzi na usalama upande wake. Wanakumbusha jinsi mwezi Machi Mutharika alivyowafukuza kazi mkuu wa majeshi na makamu wake na kuchagua wale aliowaona kuwa watamuunga mkono.

Wanasema kwa bahati, vyombo vya ulinzi na usalama vya Malawi vinajulikana kwa kuwa upande wa wananchi hasa pale inapotokea mvutano katika kubadilishana madaraka kutoka chama kimoja kwenda kingine.

Mwishoni wachambuzi hawa wanauliza kwanini ushindi huu wa upinzani umepatikana hivi sasa na sio kabla. Kwamba imekuwaje mara tu taasisi na mifumo inayoendesha uchaguzi - vyombo vya ulinzi na usalama, mahakama, tume za uchaguzi nk - imesimamia demokrasi na kutoa fursa kwa upinzani kushinda.

Wanasema utafiti zaidi utahitajika kufanyika kujibu swali hilo, lakini hapa ndipo wanaporudi kule katika hoja ya nguvu ya umma.

"Moja ya sababu kuu inawezekana ikawa kwamba nguvu ya umma ilizitia moyo taasisi kusahihisha matumizi mabaya ya madaraka," wanaandika Cheeseman na Matonga
Waziri wa Ulinzi wa Tanzania Dkt Hussein Mwinyi amepitishwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya chama cha CCM kugombea urais wa Zanzibar
Waziri wa Ulinzi wa Tanzania Dkt Hussein Mwinyi amepitishwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya chama cha CCM kugombea urais wa Zanzibar

Wanakumbusha pia kwamba kazi hii ya kuhamasisha nguvu ya umma si ya vyama vya siasa pekee, na kwamba asasi za kiraia zina mchango mkubwa katika kufanikisha hili.

Wanakumbusha namna asasi ya watetezi wa haki za binadamu nchini Malawi, ijulikanayo kama Human Rights Defenders Coalition, ilivyokuja na kauli mbiu ya "mwaka wa maandamano" na kufanikisha kuwaunganisha Wamalawi kukusanyika, kuandamana na kukaa pamoja kudai haki zao za kidemokrasia.

Viungo vilivyowezesha demokrasia kuchukua mkondo wake nchini Malawi si vigeni, vinajulikana. Somo linalotolewa kwa siasa za Tanzania na hata Afrika kwa ujumla ni uthubutu wa kutoka katika kuvijua tu na kuanza kufanyia kazi kwa vitendo.

Uwezekano wa 'muujiza' wa Malawi kutokea nchini Tanzania kwa uchaguzi wa Oktoba hii ni mdogo lakini safari ni hatua.



Comments