Denise Nkurunziza amuomboleza mumewe Pierre Nkurunziza
Mke wa rais wa Burundi, Denise Nkurunziza amesema mume wake Pierre Nkurunziza amekamilisha safari yake kwa Amani.
Pierre Nkurunziza amezikwa huko Gitega.
Maelfu ya raia wa Burundi awali walijitokeza katika mji wa Gitega kuuaga mwili wa aliyekuwa Rais Pierre Nkurunziza wakati unasindikizwa kwa ajili ya mazishi ya taifa chini ya ulinzi mkali baada ya kufariki mapema mwezi huu.
Nkurunziza, ambaye aliongoza nchi hiyo kwa miaka 15, aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 55 kutokana na kile ambacho serikali imesema ni ugonjwa wa moyo.
Ijumaa ilitangazwa kuwa sikukuu ya taifa kwa ajili ya mazishi ya Nkurunziza.
Watoto wa shule waliovaa sare zao na raia walijitokeza barabarani kusubiri msafara uliobeba mwili wa Nkurunziza kupita.
Uwanja wa Gitega ambapo hafla ya mazishi ilifanyika pia kulijaa raia kutoka kila pembe ya nchi hiyo, wote wakiwa wamevaa nguo za rangi nyeupe kulingana na ombi la serikali.
Katika uwanja uliokuwa umejaa maelfu ya watu, Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa mke wa rais wa Zambia ni miongoni mwa waliohudhuria mazishi ambapo BI. Nkrunziza aliweza kutoa hotuba kwa niaba ya familia.
Kikubwa alichokisema ni kumshukuru Mungu kwa miujiza aliyowatendea, kuwapa nguvu yeye pamoja na familia yake kipindi hiki kigumu wanachopitia.
"…Binafsi nimempoteza mpendwa wangu, watoto wamempoteza mzazi wao. Namshukuru Mungu kwa kutupa nguvu kwa kuwa imara kipindi hiki kigumu, baada ya kumpoteza mtu ninayempenda ghafla." - Ameliambia taifa.
Nguvu yake aliielezea kutoka kwa bibilia na kusema kwamba huu ulikuwa ni wakati wake wa kuondoka duniani.
Bi. Nkurunziza ambaye alikuwa na watoto watano, alimsifu mume wake kwa mema aliyotendea nchi hiyo na kwamba mwisho wake umekuwa mwema na kufa kifo cha amani.
Kazi nzuri
Bi. Nkurunziza alirejelea maneno ya Bwana Nkurunziza: "Alikuwa akisema kuwa ubaya sio kufa lakini kufa kwa ajili ya nchi na familia."
"Tumshukuru Mungu kwasababu hajawahi kutusaliti wala kusaliti nchi..."
Denise Nkurunziza anamshukuru Mungu kwa kumpa nguvu kipindi hiki kigumu
Denise Nkurunziza, ambaye amefanikiwa kuaga mwili wa mume wake katika halfa yake ya mwisho uwanja wa Gitega, amesema mume wake alifanya mema kwa nchi yake.
Katika hotuba aliyotoa, maneno ya Bi. Nkurunziza yamezingatia sana bibilia.
Bi. Nkurunziza ambaye pia alikuwa amelazwa kwa ugonjwa usiojulikana, alilazimika kuondoka hospitalini Nairobi, nchini Kenya siku moja baada ya serikali kutangaza kifo cha mume wake kwa ugonjwa wa moyo Juni 9, 2020.
Hata hivyo, upinzani nchini Burundi na makundi ya haki za binadamu mara kwa mara yalikuwa yakishtumu serikali ya Nkurunziza kwa kushindwa kuwa na uvumilivu na kutekeleza ukiukaji wa haki za binadamu.
Kuanzia leo jioni, bendera za taifa katika nchi za Kenya, Rwanda, Uganda na Tanzania zitapandishwa tena juu baada ya kupeperushwa nusu mlingoti kwa karibia wiki mbili kama njia moja ya kuonesha heshima kwake.
Mwili wa Nkurunziza ukiwa kwenye msafara wa kumuaga
Tutaendeleza nyayo zako
Rais Evariste Ndayishimiye amesema raia wote wa Burundi watafuata nyayo za uzalendo za waliotangulia kama alivyofanya, akiangazia aliye mrithi.
"Hatutamuaibisha. Tutafuata nyanyo zake…" Ndayishimiye amesema.
"Mimi binafsi nimempoteza mtu bora maishani, mwajibikaji wa wote, aliyejua kile ambacho kingeleta msuguano."
Watu walifika uwanja wa Ingoma kumuaga Nkurunziza
Uwanja wa Ingoma ulikuwa na watu wengi wanaomuaga hayati Nkurunziza.
Pierre Nkurunziza alikuwa nani?
Mwaka 2015, rais huyo aliyeingia madarakani baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha mauaji ya watu 300,000 , alisema kuwa hatawania tena ,nafasi hiyo ya urais kwa sababu ni kinyume na katiba.
Wafuasi wake walitetea kuwa katika uchaguzi wa mwaka 2005 alichaguliwa na bunge na si wapiga kura- na kutetea hoja hiyo katika mahakama ya katiba ya nchini humo.
Na kiongozi wa zamani wa waasi alijisifu kuwa ameleta amani katika utawala wake nchini Burundi.
Iliripotiwa kuwa maasifa wa diplomasia walifika kuzungumza na bwana Nkurunziza ambaye alikuwa nje kidogo ya mji mkuu , Bujumbura, walimkuta rais huyo akiwa analima na wanakijiji.
Comments
Post a Comment