Je ushindi wa upinzani Malawi una maana gani kwa demokrasia Afrika?

Lazarus Chakwera
Rais mteule Lazarus Chakwera akipiga kura mapema wiki hii.

Ushindi wa Lazarus Chakwera mwenye umri wa miaka 65 dhidi ya Rais aliye madarakani Peter Mutharika, una maana kubwa kwa uhuru wa mahakama nchini Malawi na Afrika kwa kuzingatia kuwa ni mhimili wa dola wenye kuhakikisha uamuzi wa wapiga kura unaheshimiwa na hakuna aliye juu ya sheria.

Si ushindi tu kwa Malawi bali kwa bara hilo zima. Mara nyingi kinachotangazwa na tume ya uchaguzi huwa ndiyo mwisho wa mchezo.

Uchaguzi huu wa marudio unafanana na uamuzi uliochukuliwa na mahakama kuu nchini Kenya katika uchaguzi mkuu wa 2017 wakati ilipobatilisha matokeo na kuamuru uchaguzi wa rais urudiwe ambapo Rais Uhuru Kenyatta aliweza kushinda tena baada ya upinzani kuususia.

Hali kama hiyo ya kususia uchaguzi, ilijitokeza katika uchaguzi wa 2015 visiwani Zanzibar ambapo Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi Jecha Salum Jecha alipoufuta uchaguzi na kuitisha uchaguzi wa marudio ambao upinzani uliususia, ukisema umepokonywa ushindi.

Matokeo ya uchaguzi kutokana na kuwajibika kwa tume limeendelea kuwa tatizo sugu barani Afrika. Katika nchi nyingi, mahakama na Tume za uchaguzi ni vyombo ambavyo wanaoviongoza huteuliwa na Rais aliye madarakani na hatimae kuelemea upande wa waliowateuwa.

Ni tume chache zinazowajibika na kuwa na uadilifu. Mfano mmoja ni nchini Gambia ambapo mnamo mwaka 2017, tume ya uchaguzi ilimtangaza kiongozi wa upinzani Adama Barrow kuwa mshindi halali dhidi ya rais aliyekuwa madarakani kwa muda mrefu Yahya Jammeh.

Lazarus Chakwera (kulia) amemshinda rais aliyemadarakani Peter Mutharika
Lazarus Chakwera (kulia) amemshinda rais aliyemadarakani Peter Mutharika

Kutokana na vizuizi vilivyowekwa na watawala ni nadra matokeo kupingwa mahakamani, chombo pekee kinachotegemewa kusimamia na kutoa haki.

Uchaguzi huu wa Malawi unairejesha tena nchi hiyo katika njia ya matumaini panapohusika suala zima la demokrasia na utawala bora.

Matumaini hayo yalifunguka mwaka 1994 wakati Dkt Kamuzu Banda aliyetawala kiimla tangu nchi hiyo ilipojinyakulia uhuru 1964, alipokubali matokeo aliposhindwa na Bakili Muluzi. Hata hivyo mnamo miaka iliofuata, Malawi imeonekana kuwa katika hatari ya kurudi tena katika ukandamizaji wa mafanikio hayo.

Sakata hilo liliibuka kufuatia kifo cha ghafla cha Rais wa tatu Bingu wa Mutharika na mkakati wa ndugu yake rais wa sasa Peter Muthariki kujaribu kumzuwia Makamu wa rais Joyce Banda kuonesha azma ya urais.

Lakini kilipomalizika kipindi cha mpito cha miaka miwili iliobakia ya marehemu Bingu 2014, Bi Banda alikabiliwa na upinzani mpya wa Peter Mutharika na hakufua dafu . Matokeo yake bibi Banda akaunda chama kipya cha People´s Party.

Ushindi wa Chakwera dhidi ya Mutharika licha ya kuungwa mkono na wapinzani wengine, unakirejesha madarakani chama kilichoasisiwa na Dkt Banda cha Malawi Congress MCP kwa mara ya kwanza , miaka 26 baada ya kuondoshwa madarakani.
Uchaguzi ulifanyika katika mazingira ya hatari ya corona
Uchaguzi ulifanyika katika mazingira ya hatari ya corona

Lilikuwa tukio la pili la mabadiliko ya kidemokrasia katika kanda ya kusini mwa Afrika baada ya nchi jirani na Malawi , Zambia , Rais wa kwanza Kenneth Kaunda kukubali kushindwa na mpinzani wake Frederick Chiluba. Zambia nayo sasa imeingia katika msukosuko unaohatarisha mafanikio hayo.

Moja wapo ya changamoto kubwa zitakazomkabili rais mteule Lazarus Chakwera atakaposhika rasmi madaraka ni kuhakiisha anajenga msingi wa kuimarisha uhuru wa Tume ya uchaguzi na mahakama kwa manufaa ya maendeleo demokrasia na utawala bora, ambayo wataalamu wanaashiria bado ni kikwazo kwa maendeleo ya raia panapohusika na haki zao za msingi.

Baada ya uchaguzi huu wa marudio Malawi , macho sasa yatakuwa yakielekezwa kwa jirani yake Tanzania ambayo itakuwa na uchaguzi mkuu mwezi Oktoba, huku wapinzani wakidai tume huru na serikali ikisema tume iliopo, ilioteuliwa na rais John Magufuli ni huru. Kiongozi huyo ameahidi uchaguzi huo utakuwa huru na wa haki.

Yote tisa, ushindi wa Chakwera na muungano wa vyama vya upinzaniumekuwa kipimo cha uwezo wa mahakama kushughulikia kesi za kupinga matokeo ya uchaguzi na kudhibiti mamlaka makubwa ya muhimili wa rais.

Ushindi huo nchini Malawi unavipa vyama vya upinzani kiwingineko barani Afrika matumaini kuwa pale upinzani unapoungana kwa dhati, ushindi unawezekana.

Comments