Huzuni wa Liverpool wa miaka 30 EPL wafikia kikomo

Mashabiki wa Liverpool wakisherehekea ushindi wa faligi ya Premia katika uwanja wa Anfield
Maelfu ya mashabiki wa Liverpool walikusanyika Anfield kusherehekea ushindi wa klabu yao baada ya miaka 30

Subira vuta kheri - Subira ya liverpool ya miaka 30 ili kushinda kombe la ligi ya England imetimia baada ya klabu ya Manchester City kupoteza 2-1 dhidi ya Chelsea na hivyobasi kuwathibitisha The Reds kuwa mabingwa wapya wa ligi hiyo.

Timu ya Jurgen Klopp ilihitaji ushindi mmoja ili kushinda ligi hiyo lakini ushindi wa Chelsea dhidi ya Manchester City una maana kwamba Liverpool haiwezi tena kufikiwa na timu yeyote ile katika jedwali.

Ni kombe la 19 la Liverpool na lao la kwanza tangu msimu wa 1989-90.

Licha ya kutakiwa kusalia nyumbani na meya wa mji huo kutokana na virusi vya corona , maelfu wa mashabiki walikongamana katika uwanja wa Anfiled kusheherekea ushindi huo.

Wengi wa mashabiki waliokongamana katika uwanja wa klabu hiyo walivalia barakoa, huku wengine wakiwasha fataki.


Baadhi ya wachezaji wa Liverpool , akiwemo kipa Alisson , beki Virgil van Dijk na kiungo wa kati Alex Oxlade Chamberlain, walisherehekea pamoja baada ya kutazama mechi hiyo ya Chelsea.

Klopp ambaye alikuwa akivalia tishati ya Liverpool na aliejawa na hisia , aliambia chombo cha habri cha Sky Sports: Sina maneno ya kuelezea, siamini. Ni zaidi ya vile nilivyofikiria kwa inawezekana kuwa mabingwa na klabu hii ni jambo maridhawa.

''Sijawai kusubiri miaka 30, nimekuwa hapa kwa miaka minne na nusu, lakini ni mafanikio makubwa , hususan baada ya likizo ya miezi mitatu kwasababu hakuna mtu aliejua kwamba tutatawazwa washindi."

Liverpool fans celebrate winning the league at Anfield
Huku mlipuko wa virusi vya corona ukiathiri maisha ya kawaida nchini England na kusababisha kusitishwa kwa muda kwa ligi ya Premia kwa miezi mitatu, mashabiki wa Red walihimili kusubiri ili kuona jinsi msimu huu utakavyokamilishwa, huku wengine wakisema huenda ukafutwa, na hivyobasi kufuta matokeo pamoja na juhudi zao katika vitabu vya rekodi.

Hatahivyo hilo halikutokea kwani Ligi ya Premia ilirudi mwezi huu na hivyobasi kuwawezesha kuibuka washindi.

Hatahivyo, kutoka na masharti yaliowekwa kukabiliana na virusi vya corona, The Reds hawataweza kusherehekea ushindi huo uliosubiriwa kwa muda mrefu na mashabiki wao, sio kama kawaida.

Baada ya kupata ushindi mkubwa wa 4-0 dhidi ya Crystal Palace siku ya Jumatano na huku wakitarajiwa kucheza dhidi ya Aston Villa siku ya Jumapili ,Julai 5 na wakisalia na mechi mbili za nyumbani - watacheza bila mashabiki.

Kufikia sasa hakuna uwezekano kwamba watasherehekea na mashabiki wakiwa juu ya basi lao katika mji huo kama ilivyo kawaida.

Hatahivyo mechi nyengine watakaporudi uwanjani itakuwa mechi dhidi ya wapinzani wao ManCity ambao walifanikiwa kuwashinda msimu uliopita.

Kufuatia ushindi wa Chelsea, mkufunzi wa City Pep Guardiola aliwapongeza Liverpool kwa kushinda taji hilo.


Walivunja rekodi msimu huu

Kushinda taji hilo ndio lililokuwa lengo la Liverpool ambayo ilikuwa imesubiri kwa muda mrefu ili kutawazwa mabingwa tena, baada ya kushinda taji hilo mara 11 kati ya 1973 na 1990.

Lakini baada ya ufanisi huo, huenda mambo yakaimarika zaidi, na kuvunja rekodi ya pointi 100 iliowekwa na klabu ya Man City.

Timu hiyo ya Klopp imefanya kampeni kali katika historia ya ligi ya Premia , kwa kujipatia pointi 86 na rekodi ya kushinda mechi 28, droo mbili na kushindwa mara moja katika mechi zao 31.

Hivyo ndivyo walivyotawala, na katika wakati mmoja waliongoza jedwali la ligi wakiwa na pointi 25- uongozi uliovunja rekodi na wa pili katika historia ya ligi ya Premia.

Ushindi wao wa taji hilo la ligi msimu huu ndio wa mapema katika rekodi, huku wakiwa wamesalia na mechi 7.

Huo sio ushindi wa mapema kwa tarehe, ni kwasababu ya kusitishwa kwa ligi ya premia kati ya mwezi Machi na Mei kutokana na mlipiuko wa virusi vya corona.

Miaka 30 ya mateso.

Premier League: Mengi yametokea tangu Liverpool kushinda ligi ya Premia kwa mara ya mwisho.

Ushindi huo wa liverpool unawakilisha wakati muhimu kwa mashabiki wake, waliokuwa wakizoea ushindi kati ya miaka ya 70 na 80, ikiwemo ushindi wa msimu wa 1972-73 na 1990-91 ambapo walishindwa kumaliza katika nafasi ya kwanza au ya pili katika ligi hiyo.

Hatahivyo hawajakosa kushinda taji katika kipindi hicho cha miaka 30, wakishinda kombe la FA, makombe manne ya kombe la ligi, kombe la vilabu bingwa mara mbili- la mwisho wakishinda chini ya ukufunzi wa Klopp - pamoja na makombe matatu ya Super na moja la ligi ya klabu bingwa duniani.

Comments