MVUA YAUA WATOTO WAWILI DAR, YAHARIBU MIUNDOMBINU NA KUZUA KERO KWA WANANCHI


Watoto wawili wamepoteza maisha kutokana na athari za mvua kubwa za masika zinazoendelea kunyesha katika jiji la Dar es Salaam.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema tukio la kwanza lilitokea Mei 8, mwaka huu, saa 9:00 alasiri maeneo ya Goba wilayani Kinondoni.

Alimtaja mtoto aliyefariki dunia ni Francis Byabato (6), baada ya kutumbukia kwenye kisima cha futi 30 kilichokuwa wazi nyumbani kwao.

Alieleza kuwa mtoto huyo alitoweka kwa siku mbili na baadaye alikutwa ndani ya kisima hicho akiwa ameshafariki dunia.

Kamanda Mambosasa alisema mtoto mwingine ambaye anakadiriwa kuwa na umri wa miaka (4-5), alifariki dunia Mei 12, mwaka huu maeneo ya Mongo la Ndege.

Alisema mwili wa mtoto huyo ulikutwa ukielea katika Mto Msimbazi ukiwa hauna jeraha lolote na umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Kadhalika, alisema, mvua hizo zinazoendelea kunyesha zimesababisha uharibifu wa baadhi ya majengo ya Shule ya Msingi Mwale iliyopo Kiwalani, Majani ya Chai Kiwalani na Shule ya Sekondari Kibasila iliyopo Manispaa ya Temeke ambayo imejaa maji na kusababisha kushindwa kuendelea na masomo.

Kamanda Mambosasa alitaja madhara mengine ni kufungwa kwa baadhi ya barabara za jiji hilo ikiwamo barabara ya Morogoro katika eneo la Jangwani.

Comments