KESI inayomkabili aliyekuwa Rais wa zamani wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na wenzake imekwama kuendelea kwa sababu mshtakiwa mmoja ambaye ni Mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga, hakuweza kufika mahakamani.
Mwanga hakufika mahakamani kwa sababu zilizoelezwa kwamba mahabusu wote wanaotoka Gereza la Segerea hawakuweza kufika mahakamani kwa sababu ya matatizo ya usafiri.
Akiiwakilisha Jamhuri, Wakili wa Serikali kutoka Takukuru, Leonard Swai, alidai mbele ya Hakimu Mkazi, Maira Kasonde kwamba shahidi wanaye, lakini hawawezi kuendelea sababu mshtakiwa mmoja hayupo.
“Mheshimiwa hatuwezi kuendelea, mshtakiwa wa tatu hayupo, sababu za kutokuwepo ni kwamba mahabusu wote kutoka Segerea Gerezani hawakuletwa kwa tatizo la usafiri,” alidai na kuomba tarehe nyingine.
Wakili wa utetezi, Richard Rweyongeza, hakuwa na pingamizi kwa kesi hiyo kuahirishwa.
Mahakama iliahirisha kesi hadi Mei 6 mwaka huu kwa ajili ya kuendelea na kusikiliza ushahidi wa Jamhuri.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga, Meneja wa Ofisi TFF, Miriam Zayumba na Karani wa TFF, Flora Rauya, ambao kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 30 katika kesi ya jinai namba 213 ya mwaka 2017.
Mashtakiwa hayo ni ya kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa dola za Marekani 173,335.
Malinzi, Mwesigwa na Nsiande wanaendelea kusota rumande kwa sababu wanakabiliwa na mashtaka ya utakatishaji fedha ambayo hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.
Comments
Post a Comment