Ferdinand kulamba dili nono United


MANCHESTER, England

BEKI wa zamani wa Manchester United, Rio Ferdinand, ni mmoja wa watu ambao klabu hiyo imeongea nao kuhusu kuwa Mkurugenzi wa Michezo wa timu hiyo kubwa nchini England.

Taarifa zilizotolewa na mtandao wa Sky Sports zilidai kuwa, Ferdinand aliyecheza Manchester United kwa miaka 12 alikutana na Mkurugenzi, Ed Woodward, kujadili uwezekano wa kuchukua nafasi hiyo ambayo haikuwahi kuwepo ndani ya klabu hiyo.

Inadaiwa kuwa Manchester United wanahitaji mtu ambaye anaifahamu vizuri timu hiyo, kitu ambacho kinamfanya Ferdinand kuwa na kigezo hicho kutokana na kukaa miaka 12 akiwa mchezaji wa kikosi hicho.

Ole Gunnar Solskjaer ambaye alisaini mkataba wa kukinoa kikosi hicho yupo tayari kufanya kazi na Mkurugenzi wa Michezo ndani ya timu hiyo, lakini imebainika kuwa hafurahishwi na uteuzi wa beki huyo.

Kwa kipindi chote alichokuwa Manchester United, Ferdinand alicheza michezo 455 na kushinda mataji sita ya Ligi Kuu, Ligi ya Mabingwa Ulaya, Klabu Bingwa ya Dunia, Kombe la Ligi mara mbili na mengine.

Comments