Mbunge wa CCM, Deo Sanga aomba Rais Magufuli aongezewe muda hadi 2030

Deo Sanga maarufu Jah People (CCM), ameshauri Rais John Magufuli kuongezewa kipindi kimoja cha uongozi ambacho badala ya kumaliza urais mwaka 2025, akae hadi mwaka 2030.


Rais wetu (Magufuli) ana maono makubwa ya kuifikisha mbali nchi yetu, hivyo aombewe awe rais wa kudumu, aongezewe kipindi kimoja hadi mwaka 2030.

“Mimi na wenzangu tutatembea nchi nzima kumuombea…ikifika mwaka 2021 wabunge tuanze kutembea nchi nzima kumuombea Rais Magufuli aongezewe muda,” alisema Sanga.

Mbunge huyo aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, alitoa maoni yake hayo wakati akichangia Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2019/2020 yaliyowasilishwa juzi na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Naye Mbunge wa Kijitoupele, Shamsi Vuai Nahodha (CCM) alisema Rais Magufuli ana maono ya kulipeleka Taifa mbali zaidi na kuachana na kupitisha bakuli kwa wafadhili kuombaomba, hivyo kuwataka Watanzania kufanya kazi kwa bidii ili Taifa lijitosheleze.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kilombero, Peter Lijuakali (Chadema) alisema “Inasikitisha wabunge wana mawazo ya kutaka Katiba ifanyiwe marekebisho makubwa ili rais aongezewe muda, inafedhehesha sana.,”

Comments