Fulham imekuwa timu ya pili kushuka daraja katika Ligi ya Primia msimu wa 2018/19 baada ya kuchapwa na Watford 4-1.
Timu hiyo bado ina michezo mitano mkonononi, lakini kwa alama zake 17 mkononi haiwezi tena kumaliza katika nafasi salama.
Fulham sasa inaungana na Huddersfield wenye alama 14 ambao walikuwa wa kwanza kushushwa daraja.
Watford ilikuwa ya kwanza kupata goli katika mchezo huo, lakini Ryan Babel alirudisha matumaini ya Fulham kabla ya mapumziko. Fulham walikuwa wanahitaji walau suluhu katika mchezo wa leo ili kuendelea kupambania kubaki ligi kuu kwenye michezo iliyosalia.
Hata hivyo kipindi cha pili kilikuwa kigumu zaidi kwao ambapo waliruhusu magoli matatu kutoka kwa Will Hughes, Troy Deeney na Kiko Femenia.
Fulham ilitumia kiasi cha pauni milioni 100 kununua wachezaji 12 mwanzoni mwa msimu lakini bado kikosi hicho kimekosa ubora na umakini msimu mzima.
Baada ya kipyenga cha mwisho kupulizwa wachezaji wa Fulham walikuwa taabani kwa uchovu na fikra za kuwa msimu ujao watacheza ligi ya chini.
Msimu huu ndio umekuwa wa kwanza kwa timu mbili kushushwa daraja kufukia Aprili 2.
Kinyang'anyiro sasa kipo katika nafasi ya moja ya mwisho kwa timu tatu zinazotakiwa kushuka daraja.
Cardiff ndio wamo hatarini zaidi na alama zao 28. Lakini wangali na michezo saba mkononi.
Timu nyengine ambazo zimo hatarini ni Burnley, Southampton na Brighton ambazo zote zina alama 33.
Manchester United yachapwa
Wolves wakisawazisha katika dakika ya 25 kupitia Diogo Jota.
Matumaini ya Manchester United kumaliza katika nafasi nne za juu yameingia dosari Jumanne usiku baada ya kukubali kichapo cha goli 2-1 kutoka kwa Wolves.
Sasa United kwa mujibu wa kocha wao itawalazimu kushinda mechi tano kati ya sita zilizosalia ili kumaliza katika nafasi nne za juu na kupata tiketi ya kucheza ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.
United walikuwa wa kwanza kupata goli katika dakika ya 13 kupitia kiungo Scott McTominay, lakini Wolves walisawazisha katika dakika ya 25 kupitia Diogo Jota.
Msumari wa mwisho katika jeneza la United uligongelewa kwa goli la kujifunga kupitia kwa beki Chris Smalling katika dakika ya 77.
United walicheza wakiwa 10 toka dakika ya 57 ya mchezo baada ya Ashley Young kutolewa kwa kdi nyekundu.
Sasa klabu hiyo imesalia katika nafasi ya tano wakiwa na alama 61, alama 2 nyuma ya Arsenal waliopo nafasi ya tatu, alama sawa na Tottenham ambao wapo nafasi ya nne na alama moja juu ya Chelsea waliopo nafasi ya 6.
Hata hivyo, United wamecheza mchezo mmoja zaidi ya klabu zote hizo za London. Hiyo inamaanisha kuwa endapo Chelsea watawafunga Brighton leo usiku itawashusha United mpaka nafasi ya 6.
Comments
Post a Comment