Imetimia miaka 47 tangu Rais wa kwanza wa Z’bar, Hayati Karume aage dunia, hivi ndivyo hali ilivyokuwa siku aliyofariki

Leo April 7, 2019 inatimia miaka 47 ya kifo cha Rais wa kwanza wa Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume aliyezaliwa 1905 na kufariki 7/4/1972, kwa kupigwa risasi. Aliiongoza Zanzibar kuanzia 1964 baada ya Mapinduzi.

Sheikh Abeid Amani Karume aliuawa kwa kupigwa risasi katika jengo la Makao Makuu ya Chama cha Afro-Shirazi (ASP) visiwani mjini Zanzibar mnamo tarehe 7 Aprili, 1972.

HAYATI ABEID AMANI KARUME

Mara tu baada ya mauaji hayo kufanyika hali ya hatari ilitangazwa nchi nzima ikifuatana na msako mkali uliohusisha watu kadhaa kutoka katika vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na raia huku taarifa zikimtaja Abdulrahman Muhammed Babu kuwa  muhusika mkuu.

Hadi leo hii hakuna ukweli thabiti juu ya kifo cha Hayati Karume maana wengine wanahusisha kifo chake na chuki za siasa na mengineyo.

Japokuwa Mjane wa Karume (Bi. Fatma Karume) anasema hakuwa akifahamu kifo cha Mzee Karume mpaka alipokuja kuambiwa na mdogo wake kuwa ameona gari ya mzee imetoka bila ya kuwa na mtu ndipo alipojaribu kumpigia Kamishna wa Polisi enzi hizo Mzee Kisasi lakini hakufanikiwa kumpata kwa kuwa naye alikuwa ameshaenda hospitalini alipokuwa amehifadhiwa baada ya kupigwa risasi.


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na mjane wa Mzee Karume, Mama Fatma Karume wakati alipomtembelea nyumbani kwake.

“Akaja mdogo wangu masikini marehemu kwa sasa, akaniambia dada nimetoka huko nje kubaya kuna risasi zinalia lakini nimekuta gari ya mzee inakwenda huko, mzee hayupo kwenye gari. Mimi nikajikaza nikamwambia hapana mzee hawezi kutumia gari hiyo sasa hivi pengine wametua gari nyingine kumuondosha. Nikampigia simu kisasi alikuwa Kamishna wa Polisi kipindi hicho lakini akapokea mke wake na kuniambia mzee hayupo ameenda kwenye tukio hili lililotokea, nikamuuliza wapi akaniambia hospitali nikaingiwa na mashaka nikaanza kukumbuka aliyoniambia mdogo wangu”. Alisema Bi. Fatma Karume

Aidha Bi. Fatma amesema alipofika katika hospitali ya Muungano alizuiliwa kuingia ndani na wanajashi waliokuwa wametanda eneo hilo kwa bahati nzuri mwanaye Haji Mrisho naye alikuwa ni miongoni mwa wale wanajeshi akapata wepesi wa kuingia na kumuona Karume akiwa amelazwa chini ameshafunikwa shuka.


Pamoja na hayo amesema siku ya maziko aliweza kuonana Mwalimu Nyerere wakakumbatiana lakini hakuweza kujua kilichoendelea hapo kwa kuwa alipoteza fahamu kutokana na majonzi aliyokuwa nayo.

Kwa vyovyote vile, jina la Abeid Karume haliwezi kusahaulika katika historia ya ukombozi visiwani humo kutokana na misingi aliyowajengea Wazanzibar.

Comments