Tanzia : MTANGAZAJI WA CLOUDS FM KIBONDE AFARIKI...ALIKUWA MC KWENYE MSIBA WA RUGE



Mtangazaji wa Clouds FM Ephraim Samson Kibonde, amefariki dunia Alfajiri ya leo Machi 7, 2019 akiwa mkoani Mwanza.

Kibonde ambaye alikuwa MC kwenye msiba wa Ruge amekutwa na umauti kwenye hospitali ya Bugando mkoani Mwanza.

Mtangazaji huyo alikuwa miongoni mwa waombolezaji waliomsindikiza Ruge hadi katika maziko yake wilayani Bukoba.


Mtangazaji na Meneja Ubunifu wa Clouds, Siza ameeleza kuwa Ephrahim Kibonde alianza kuumwa tu ghafla baada ya kuendesha shughuli nzima ya kuuzika mwili wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds, Marehemu Ruge Mutahaba.

 Siza amesema baada ya Kibonde kuendesha shughuli nzima nyumbani kwa kina Ruge mjini Bukoba alianza kujisikia vibaya akiwa eneo hilo hilo la msiba na kusaidiwa na watu wa msalaba mwekundu wakisaidiana na Dk Issac Maro wa Clouds.

Amesema baada ya hilo kumtokea aliingizwa ndani ya nyumba ya kina Ruge na kuvuliwa viatu pamoja na kulegezwa mkanda kwa kuwa ilionekana kama amepatwa na presha hivyo akapewa huduma ya kwanza akiwa hapo hapo nyumbani.

“Baada ya huduma ya kwanza tulimpeleka katika hospitali ya Bukoba kwa kuwa hali yake haikuwa nzuri hivyo akatibiwa pale na kupata chakula hivyo akarudi katika hali nzuri kidogo,”amesema Siza.

Amesema kuwa baada ya Kibonde kupata nafuu Dk Issac na wenzake walijadiliana na madaktari wa hospitali ya Bukoba kama Kibonde anaweza kusafiri hadi Mwanza kwa ajili ya matibabu zaidi.

“Baada ya majadiliano tulimuuliza Kibonde kama anaweza kusafiri hadi Mwanza kwa kuwa ndege yetu ilikuwa inaondoka asubuhi hivyo alisema anaweza na tukakukabiana tukampeleka uwanja wa ndege kwa safari,”amesema Siza.

Amesema kuwa walifanikiwa kufika Mwanza na walimweka Kibonde kwenye wheel chair akisaidiwa na Dk Issac ambaye alikutana na mwenzake ambaye ana hospitali Mwanza.

“Baada ya kufika pale tulimwacha Kibonde na Dk Issac na hiyo daktari mwingine ambaye ni rafiki yake sisi tukaendelea na safari kuelekea Dar es Salaam hadi leo asubuhi tunapata taarifa kuwa amefariki hivyo ndivyo ilivyokuwa,”amesema Siza.

Kwa mujibu wa Sebastian Maganga, taratibu zinafanyika kupanga mipango ya msiba huo.


Comments