Rais Mstaafu Kikwete aguswa na kifo cha Ephraim Kibonde


Rais Mstaafu Jakaya Kikwete ameonyesha kuguswa na kifo cha Mtangazaji wa Clouds FM, Ephraim Kibonde.

Kifo cha mtangazaji huyo wa kipindi cha Jahazi kimekuja siku chache baada kufariki Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji Clouds Media,Ruge Mutahaba.

"Majonzi yangali nasi, nimepokea taarifa ya kifo cha Mtangazaji Ephrahim Kibonde wa Clouds FM. Ni pigo kubwa kwetu sisi wapenzi wa kipindi cha Jahazi. Jahazi litaeleaje bila ya Nahodha Kibonde? Mwenyezi Mungu na aipe faraja familia yake, Clouds FM na wasikilizaji wote wa Jahazi," ameandika Kikwete kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Wakati huo Mkurugenzi wa Clouds Media Group, Joseph kusaga amesema kuwa mwili wa marehemu utawasili na kupokelewa leo katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere saa nne usiku na baada ya hapo utapelekwa katika hospitali ya Jeshi Lugalo kwa ajili ya kupumzishwa.

Vilevile amesema amesema taratibu za mazishi na maombolezo zitafanyika nyumbani kwake Mbezi na siku ya jumamosi ataagwa rasmi na kuzikwa.

Comments