Mwili wa kijana mwenye umri wa miaka 25 umepatikana katika msitu wa Katangara chini yake kukiwa na Biblia, huku ukiwa umevaa rozari shingoni na umepiga magoti.
Kijana huyo, Godwin Massawe, mkazi wa Kijiji cha Msaranga wilayani Rombo ambaye alitoweka Jumapili ya Januari 20 baada ya kuaga kuwa anakwenda kanisani, mwili wake ulikutwa porini Machi Mosi.
Baba mzazi wa kijana huyo, Frimin Massawe aliliambia Mwananchi jana kuwa, baada ya mwanaye kutoweka alitoa taarifa polisi na kanisani ili asaidiwe kupatikana kwake.
“Tulipeleka taarifa polisi mpaka kanisani, lakini hatukufanikiwa. Jana (juzi) nililetewa taarifa na wazee wanaopasua mbao katikati ya msitu (wa Katangara) wakasema kuna mtu ameonekana amefariki (dunia) muda mrefu,” alisema Massawe.
Alisema watu hao walimweleza kuwa marehemu amepiga magoti akiwa na Biblia huku amevaa rozari, ndipo alipoongozana nao kwenda polisi na baadaye msituni.
“Tukafika hadi Katangara na kuingia ndani (ya msitu) mwendo wa saa nne. Kule kulikuwa na baridi kali sana na wanyama wakali, lakini bado niliona maajabu ya Mungu.”
Alisema, “Huwezi amini nilimkuta mwanangu Godwin amepiga magoti kwenye gogo akiwa na rozari yake shingoni na Biblia ipo chini imefunguliwa kitabu cha Joshua huku akiwa ameoza.”
Mzazi huyo alisema mabaki ya mwili huo yalikuwa hayatoi harufu, jambo alilodai kuwa ni ‘muujiza’.
Baba mdogo wa marehemu, Simon Massawe alisema tukio hilo limewashangaza na kama familia wameumia kwa kuwa kijana wao alikuwa mtu wa maombi muda mwingi.
“Sisi kama familia tumelipokea kwa huzuni kubwa, hatukutegemea kumkuta amekufa. Ila kama amekufa kiimani let it be (acha iwe hivyo),” alisema.
Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Hamis Issah alisema mwili wa kijana huyo umehifadhiwa katika Hospitali ya Huruma iliyopo wilayani Rombo.
Comments
Post a Comment