'Ivory Queen': Mahakama Tanzania yamfunga 'malkia wa pembe za ndovu' Yang Feng Glan na wenzake miaka 15 jela
Malkia wa Pembe amefikishwa katika mahakama ya Kisutu leo
Raia wa China Yang Feng Glan anayefahamika kama 'Ivory queen' na washtakiwa wengine wawili wamehukumiwa miaka 15 jela baada ya kupatikana na hatia ya kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo.
Bi Feng na wengine, Silvanus Matembo, na Philemon Julius Manase waliofikishwa hii leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wametiwa hatiani kwa mashtaka matatu, yanayohusu ulanguzi wa meno ya tembo ikiwemo uhujumu uchumi.
Watatu hao walipandishwa kizimbani kujibu mashtaka yahusianayo na biashara ya meno ya tembo yenye thamani ya takriban dola milioni 6
Katika shtaka la pili la uhujumu uchumi, watatu hao wamefungwa miaka miwili ama kulipa faini ya faini ya thamani ya mara mbili ya nyara walizovuna.
Jumla ya kifungo chao ni miaka 17 lakini watatumikia miaka 15 jela.
Mahakama imeeleza kwamba ushahidi umetolewa na watu 11 wakiwemo wasafirishaji.
Ulanguzi wa Pembe za tembo umechangia kuongezeka kwa visa vya uwindaji haramu
'Ushahidi wote unaonyesha jinsi gani nyinyi( washtakiwa) mmefahamiana kwa muda mrefu' amesema jaji Huruma Shaidi.
''Ushahidi unaonesha jinsi gani washtakiwa wote watatu walivyosaidiana kuhakikisha wanatafuta meno ya tembo sehemu mbalimbali na kuyasafirisha'' ameongeza jaji Shaidi.
Waendesha mashtaka wamebaini kwamba Bi Feng aliidhinisha mtandao wa kihalifu na kufanikiwa kusafirisha meno ya tembo katika maenoe tofuati kwa kutumia mgahawa wake wa vyakula vya Kichina kujificha na hata kutishia kuwaua watu katika kuidhibiti biashara hiyo haramu.
Kwa mujibu wa wanaharakati, hii ni kesi kubwa inayohusu ulanguzi wa pembe za ndovu kuwahi kushuhudiwa Tanzania.
Mnamo mwaka 2015, jopo maalum la maafisa wanyama pori nchini Tanzania liliwakamata Bi Feng miongoni mwa wengine walioshukiwa kusafirisha pembe za ndovu.
Makundi ya kampeni dhidi ya uwindaji haramu yalieleza kuwa wale waliokamatwa ni pamoja na mwanamke aliyepewa jina la utani 'Malkia wa pembe za ndovu' Yang Feng Glan.
Wahifadhi wameitaja Tanzania kama shina la uwindaji haramu wa pembe za ndovu.
Feng anaonekana kama nguvu ya nyuma katika biashara hiyo haramu ya uwindaji haramu wa pembe au meno ya tembo, na magengi ya ulanguzi kwa takriban miongo miwili iliyopita.
Bidhaa hizo hutolewa nchini Tanzania na kusafirishwa katika eneo la Mashariki mwa dunia.
'Malkia wa Pembe za ndovu' ni nani?
Waendesha mashtaka wanasema Yang Feng Glan, anayejulikana kwa umaarufu pia kama Malkia wa pembe, aliendesha biashara haramu ya kuwaua ndovu katika mbuga za wanyama ili kupata pembe zao ambazo wanazisafirisha na kuziuza katika mataifa ya bara Asia.
Lakini tunafahamu nini kumhusu?
Ametoka Beijing, Bi Yang alifika Tanzania kwa mara ya kwanza katika miaka ya 70.
Ni mwanafunzi wa kwanza wa Kichina aliyefuzu Kiswahili.
Amefanya kazi kama mkalimani katika shirika la reli Tazara lililojengwa kwa usaidizi wa China.
Inaarifiwa kwamba baada ya ujenzi wa reli hiyo mnamo 1975 alirudi Beijing kufanya kazi katika idara ya biashara ya nje.
Mnamo 1998 aliamua kuanzisha biashara Tanzania.
Alikodisha jengo la orofa mbili Dar-es-Salaam, na kufunguwa mgahawa wa vyakula vya Kichina katika sehemu ya chini ya jengo na kufungua kampuni ya uwekezaji, Beijing Great Wall Investment, katika gorofa ya juu.
Anashutumiwa kwa kuendeleza shughuli hiyo kwa takriban miaka 14.
Maafisa wa serikali Tanzania walitaja kukamatwa kwa Yang Feng Glan kama ufanisi mkubwa.
Taifa hilo la Afrika mashariki limepoteza thuluthi mbili za ndovu wake katika kipindi cha miaka kumi iliyopita.
Comments
Post a Comment