Barrick, Tanzania waafikiana kuhusu malipo ya $300 milioni

makinikia
Rais Magufuli akitete na Dkt Willem Jacobs kutoka Barrick
Kampuni ya Barrick Gold na Serikali ya Tanzania leo Jumatano Februari 20 wamefanya mazungumzo juu ya utekelezwaji wa makubaliano ambayo pande hizo mbili waliingia mwaka 2017.

Kampuni hiyo ambayo ni mmiliki wa kampuni ya Acacia ambayo iliingia kwenye mzozo na serikali ya Tanzania juu ya usafirishwaji wa mchanga wa madini au makinikia na kukwepa kodi.

Acacia imeendelea kukana tuhuma zote dhidi yake lakini mzozo huo ukiendelea kufukuta, uongozi wa Barrick chini ya mwenyekiti wake Prof John Thornton walijitosa kwenye mazungumzo na serikali ya Tanzania.

Mwezi Oktoba 2017, pande hizo mbili ziliafikiana kuwa kampuni hiyo kuilipa Serikali ya Tanzania hisa ya asilimia 16 na mgawo wa asilimia hamsini ya mapato ya mauzo ya dhahabu kutoka migodi 3 inayoimiliki..

Barrick pia walikubali kutoa Dola za Kimarekani milioni 300 kama malipo ya kuonesha nia njema ya kufidia fedha zilizotokana na upotevu wa mapato kutokana na biashara ya kampuni hiyo.

Makubaliano hayo hata hivyo hayajatekelezwa, na kulishughulikia hilo, hii leo Afisa Mwendeshaji Mkuu wa Barrick anayeshughulikia Africa na Mashariki ya Kati Dkt Willem Jacobs amekutana na Rais Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam.
Kikao Magufuli na Barrick
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, Waziri wa Katiba wa Tanzania Profesa Palamagamba Kabudi mbaye ndiye aliyeongoza mazungumzo ya suluhu amesema wanatarajia utekelezwaji wa makubaliano hayo kufikia mwishoni mwa mwezi Machi 2019.

"…sasa ni kwa kila upande kwenda kwenye vyombo vyake vinavyohusika kufanya maamuzi ya mwisho ili utekelezaji ufanyike," amenukuliwa Prof Kabudi kwenye taarifa ya Ikulu.

Hata hivyo kwa upande wake, kampuni ya Barrick katika taarifa yao hawajataja ni lini hasa maafikiano hayo yatafanyiwa kazi.

Katika taarifa yao wamesema kuwa watawasilisha makubaliano yao kwa "wakurugenzi huru" wa Acacia hivi karibuni ili wayafanyie kazi.

Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Barrick Mark Bristow amenukuliwa kwenye taarifa hiyo akisema kuwa mzozo huo umekuwa na athari kubwa kibiashara na wanaamini kuwa utekelezwaji wa makubaliano hayo utakuwa na tija kwa pande zote.

Comments