John Magufuli: Utayakumbuka zaidi matukio gani ya rais wa Tanzania kwa mwaka 2018?

Rais John Magufuli

Tanzania imepokea ndege yake ya kwanza aina ya Boeing 787-8 Dreamliner mwezi Juni 2018. Ndege ya pili kama hiyo yatarajiwa kuwasili 2020.
Mwaka 2018, umefikia ukingoni na Rais John Pombe Magufuli amekuwa na mwaka wenye matukio tele ya kukumbukwa, je wewe utamkumbuka zaidi kwa lipi?
Mwezi huu wa Disemba, amepokea ndege ya tano toka alipoingia madarakani miaka mitatu iliyopita. Katika hafla ya mapokezi iliyofanyika kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam, furaha ya rais Magufuli ilikuwa iwazi.

Akikamatana mkono na Waziri Mkuu wake, Kassim Majaliwa walisakata rhumba kabla ya kwenda kupiga ngoma. Ilikuwa ni tarehe 23 na yalikuwa ni mapokezi ya Airbus Airbus 220 - 300.

Kati ya ndege saba ambazo serikali ya Magufuli iliazimia kununua, tatu ni ndogo aina ya Bombardier Q400 ambazo zote zimeshawasili Tanzania na zinafanya kazi, na mbili ni za masafa ya kati aina ya Airbus amabayo moja imeingia mwezi huu na nyengine moja inatarajiwa kuingia mapema mwakani.
Ndege mbili ni kubwa na za masafa marefu aina ya Boeing 787-8 Dreamliner, tayari moja imewasili mwezi Juni mwaka huu na ya pili inatarajiwa kuingia Tanzania 2020.

Wakati akiipokea ndege hiyo kubwa Magufuli alisema: "Tumefufua ATCL kurejesha heshima ya nchi, ilikuwa aibu kutokuwa na ndege kwa nchi kubwa kama Tanzania ... Tangu tumeongeza ndege 3 mpya aina ya Bombardier Q400 biashara ya ATCL imeongezeka, Shirika letu lilikuwa linasafirisha abiria 4,000 tu kwa mwezi lakini sasa linasafirisha abiria 21,000 na ndege zinatua katika vituo 12."
Magufuli pia alitupilia mbali kuwa ununuzi wa ndege hauna manufaa kwa watu walio wengi: "Ndege zote hizi tumenunua kwa fedha zetu wenyewe, hatujakopa kwa mtu...Madai kuwa Watanzania wengi hawafaidiki na ndege hayana msingi. Wapo wengi wanaohitaji ndege bei ilikuwa juu."

quote box

Wapinzani kuishia jela
Toka alipoingia madarakani miaka mitatu iliyopita, masikilizano baini ya rais Magufuli na viongozi wa vyama vya upinzani si mazuri.
Wakati Rais Magufuli akivituhumu vyama hivyo kupinga kila kitu hata miradi ya maendeleo na bajeti wapinzania wamekuwa wakimtuhumu kuwa ni dikteta.
Mwezi Novemba, Magufuli alituma salamu kwa upinzani akiwaonya kuishia jela iwapo 'hawataheshimu sheria'.

Salamu hizo alizituma kupitia Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa ambaye sasa ni kiongozi muandamizi wa chama cha upinzani cha Chadema.
Magufuli na Lowassa walikutanaJumanne Novemba 27 katika ufunguzi wa maktaba ya kisasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

"...Nimeona hili nilizungumze kwa heshima kubwa, Mzee Lowassa ili wale unaowaongoza kule, uende ukawashauri, otherwise (lasivyo) wataishia magereza ili wakajifunze namna ya kuheshimu sheria za Watanzania."

Wakati akiyasema hayo, tayari Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Upinzani Bungeni Freeman Mbowe na Mbunge Tarime Mjini Esther Matiko walikuwa wamefutiwa dhaman kwenye kesi inayowakabili na mpaka wa leo (Disemba 28) bado wanashikiliwa mahabusu kwenye gereza la Segerea.
Image result for maalim seif images
Maalim Seif: Yanayotokea chini ya Magufuli, hatujawahi kuyaona Tanzania

Vyama sita vya upinzani vimewatangaza kwenye azimio lao la mwezi huu kuwa viongozi wawili hao ni wafungwa wa kisiasa.
Viongozi wa vyama hivyo wameahidi kuungana na kuutangaza mwaka 2019 kuwa ni 'Mwaka wa Kudai Demokrasia', na kadhalika wakaahidi kufanya mikutano ya siasa bila kujali katazo la mikutano ya hadhara.
"Ni mwaka ambao tutapambana kuzidai haki zetu zote tunazonyimwa kinyume na sheria na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania," taarifa ya pamoja ya viongozi wa vyama hivyo inasema.
"Kama vyama vya siasa vyenye uhalali na vyenye utaratibu uliowekwa rasmi kisheria na kikatiba, tutatangaza rasmi namna na utaratibu wa kufanya mikutano yetu ya hadhara katika kila kona ya nchi yetu, hatutaruhusu katazo haramu na lisilo na mashiko ya kisheria litumike kutuzuia kutekeleza wajibu wetu."


Vyama vilivotia saini 'Azimio la Zanzibar' ni CUF, NLD, Chadema, Chaumma, NCCR Mageuzi na ACT Wazalendo.
Masharti ya mikopo na misaada
Katika hafla hiyo hiyo ya kuzindua maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Magufuli aliwasifu Wachina kuwa wanatoa misaada isiyokuwa na masharti.
Ujenzi wa maktaba hiyo umegharimu shilingi bilioni 90 ambazo ni msaada wa serikali ya Uchina: "..."China ni marafiki wazuri wametoa zaidi ya Bilioni 90 fedha za walipa kodi wao bila masharti, maana wengine wangetoa masharti...Jambo la kufurahisha ni kwamba misaada yao haiambatani na masharti. Wenyewe wakiamua kukupa wanakupa, walitujengea TAZARA, URAFIKI na pia wametusaidia katika maeneo mengine ya maendeleo."
Masharti ya Benki ya Dunia ya mkopo kwa Tanzania
Magufuli na Balozi China Wang Ke
Rais Magufuli amemhakikishia Balozi wa China Wang Ke kuwa serikali ya Tanzania itahakikisha kila msaada unaotolewa unatumiwa vizuri.

Mwaka huu Tanzania imepitia wakati mgumu kwenye suala la masharti ya misaada na mikopo.

Benki ya Dunia imezuia mkopo wa dola milioni 300 wa kuboresha elimu ya sekondari ikitaka serikali ya Tanzania ibadili sera yake ya kuzuia wanafunzi wa kike kuendelea na masomo baada ya kujifungua.
Serikali ya Denmark imezuia msaada wa dola milioni 10 baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda kutoa kauli kali dhidi ya wapenzi wa jinsia moja.

Uzazi wa mpango

Mwezi Septemba, rais Magufuli aliwashauri wanawake waache kutumia dawa za kupanga uzazi akisema kuwa nchi inahitaji watu zaidi.

"Wanawake sasa wanaweza kuacha kutumia dawa za kupanga uzazi," Rais wa Magufuli alisema.
"Magufuli alitoa matamshi hayo akiwa ziarani wilayani Meatu akisema watu wanaotumia dawa za kupanga uzazi ni wavivu.

Hawataki kufanya kazi kwa bidii kulisha familia kubwa. Ndiyo sababu watu huamua kutumia njia za kupanga uzazi na kumalizia na mtoto mmoja au wawili," alisema.

Kwa kawaida mwanamke nchini Tanzania huwa na watato zaidi ya watano
Kwa kawaida mwanamke nchini Tanzania huwa na watato zaidi ya watano

"Nimesafiri Ulaya na kwingineko na nimeona athari za kupanga uzazi. Nchi zingine sasa zinakumbwa na upungufu kwa watu."

Rais Magufuli alitoa matamshi kama hayo mwaka 2016, baada ya kuzinduliwa mfumo wa elimu ya bure ya shule ya sekondari: "Wanawake sasa wanaweza kutupa dawa zao za kupanga uzazi. Elimu ni bure."

Waziri wa Afya akalainisha kauli hiyo akaisema "rais alikuwa akitania watani zake (kabila la) Wazaramo," lakini safari hii Magufuli alisema hataki kusikia watu wakisema kuwa "nilikua natania, sitanii."

Ununuzi wa korosho

Katika hali ambayo haikutarajiwa na wengi, rais Magufuli alitiangaza Novemba 12 kuwa Serikali kupitia Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) itanunua korosho zote kutoka kwa wakulima.
Hatua hiyo ilifuata baada ya serikali kutoafikiana na wafanyabiashara ambao hawakufikia kiwango cha shilingi 3,000 kwa kilo.

Mzozo ulianza baada ya wakulima katika mikoa ya kusini kugomea bei kati ya Sh shilingi 1,900 hadi 2,700 kwa kilo. Serikali iliungana na wakulima na baada ya kukutana na waafanyabiashara kwenye kikao ambacho rais Magufuli alishiriki bei ya kuanzia shilingi 3,000 'ikakubaliwa', lakini utekelezaji wake haukufanikiwa.

Mwaka jana kilo ya korosho ilifikia kuuzwa mpaka kwa shilingi 5,000 kwa kilo.
Baada ya amri ya rais, wanajeshi walianza kutekeleza 'Oparesheni Korosho' na walielekea mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma kulinda maghala na kusafirsha zao hilo.

Sakata hilo pia liliwang'oa uongozini waziri wa kilimo Charles Tizeba na waziri wa biashara Charles Mwijage.

korosho
Kumekuwa na maoni tofauti juu ya hatua hiyo ya kulihusisha jeshi, wapo wanaosifu na wengine wakikashifu na kulaumu.

Mnamo mwezi Juni mjadala mkali ulizuka nchini Tanzania kuhusu mapendekezo ya bajeti ya mwaka 2018 /2019 katika zao la korosho. Mapendekezo hayo ni pamoja na kuondolewa kwa ruzuku ya asilimia 65 iliyokuwa inaenda kwenye Mfuko wa Maendeleo wa Korosho na badala yake, iende kwenye mfuko mkuu wa serikali.

Ingawa mapendekezo hayo yalipita, wabunge wa mikoa ya kusini bila kujali tofauti za kisiasa waliungana kupinga. Walifikia hatua ya kutishia kuandamana.
Rais Magufulia akajibu kuwa laiti wangeliandamana na kuzua ghasia basi angewatuliza kwa kutumia vyombo vya usalama.

Alimwambia waziri mkuu Majaliwa ambaye anatokea Lindi kuwa angalianza na shangazi yake kama maandamano yangefanyika.

Stiegler's Gorge
Tarehe 12 Disemba, Tanzania ilisaini mkataba wa ujenzi wa bwawa la kufua umeme katika mto Rufiji eneo la Steigler's Gorge.

Mradi huo umekuwa ukitajwa na kusahaulika kwa miaka 40 sasa toka wakati wa rais wa awamu ya kwanza Mwalimu Nyerere.

Sabubu kuu mbili ambazo zimekuwa zikielezwa kuzuia mradi huo zilikuwa ni uhaba wa fedha na kulinda mazingira. Eneo la mradi lipo ndani ya hifadhi ya pori la wanyama la Selous.
Rais Magufuli amesema kutekelezwa kwa mradi huo ni jambo la lazima iwapo Tanzania inaazimia kujenga uchumi wa viwanda kwa kuwa umeme wa maji "ndio wa bei nafuu zaidi."
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa pamoja na Balozi wa Misri Tanzania, Mohamed Gaber Mohamed Abulwafa

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa pamoja na Balozi wa Misri Tanzania, Mohamed Gaber Mohamed Abulwafa

Mradi unakadiriwa kutumia shilingi trilioni 6.5 sawa na dola bilioni 2.9 na ukikamilika utazalisha megawati 2,100.

Mfuko wa Mazingira wa Kimataifa (WWF) umeshatoa ripoti inayoonyesha madhara ya kimazingira na uhifadhi wa mradi huo.

"Kuna matokeo makubwa zaidi ya mafuriko ya kilometa za mraba 1,200 za eneo linalohitajika na ujenzi wa bwawa hilo. Kutakuwa na ongezeko la mmomonyoko wa ardhi utakaosababisha kukauka kwa vyanzo vya maji yanayotegemewa na wanyamapori, hivyo kuathiri sekta ya utalii.

"Itapunguza rutuba katika ardhi na mazingira ya delta ya Rufiji na upatikanaji wa samaki aina ya kamba kochi na samaki wengineo wanaopatikana katika eneo hilo na hivyo kuathiri maisha ya wananchi wapatao 200,000 wanaoishi maeneo hayo," imesema ripoti hiyo.

Comments