Watoto wakipokea mafunzo darasani
Kuna maswali mengi ambayo yamezuka baada ya wizara ya elimu nchini Kenya kusongeza mbele utekelezwaji wa kitaifa wa mtaala mpya wa elimu hadi mwaka wa 2020.
Hata hivyo, waziri wa elimu nchini Kenya Amina Mohamed, anasemekana kuipuuza ripoti ya wataalamu maalum wa wizara ya elimu kuhusiana na utekelezwaji wa mtaaala huu mpya ambayo ilionyesha kuwa Kenya ilikuwa tayari kutekeleza mtaala mpya wa mfumo wa 2-6-3-3.
Katika ripoti hiyo, waziri alikuwa ameonyesha kuwa vitabu 219 vilikuwa vimepitiwa na kupitishwa kwa matumizi ya nasari na madaraja ya 1 hadi ya 3).
Pia waziri alikuwa ameeleza kuwa wizara yake ilikuwa imetoa mafunzo kwa walimu wanaofundisha viwango vya chini katika maeneo 1,168. Eneo moja la elimu nchini Kenya lina shule za msingi 20.
Aidha ripoti hiyo ilionyesha kuwa kulikuwa na watoa mafunzo wa hali ya juu wapatao 71, watoa mafunzo 507, watoa mafunzo kieneo 3,360, walimu wa shule za msingi wapatao 96,522 nawalimu wa chekechea 79,760 ambao walikuwa wamepata mafunzo kwa mtaala mpya.
Mtaala mpya ulikuwa utekelezwe katika kiwango cha nasari hadi darasa la tatu huku majaribio yakianza kwenye darasa la nne mwaka ujao. Hii ni baada ya majaribio kuwepo kwa madarasa ya chini kwa miaka mwili.
Hata hivyo, katika kufikia hatua ya kusimamisha utekelezwaji wa mtaala alitumia ripoti ya wakaguzi wan je ambayo ilionyesha mianya inayoweza kutoa changamoto katika utekelezaji wa mtaala mpya. Hatua hii imefanya chama kikuu cha walimu nchini Kenya (KNUT) kuiuliza wizara ya elimu kuanza upya shughuli yenyewe ya kuutekeleza mtaala mpya. Tayari chama cha Knut kimeitisha mgomo mwakani kutokana na masuala mengine yanayohusu walimu.
Kulingana na wizara ya elimu nchini Kenya, hatua hii imechukuliwa kwa sababu hakukuwa na matayarisho ya kutosha kuhusiana na mtaala huo na kutekelezwa kwa haraka kungeanza mwezi ujao kungekumbwa na changamoto nyingi.
Kamati ya kitaifa inayojumuisha wataalamu kutoka sekta mbalimbali iligundua matatizo mbali mbali ambayo yamefanya kuhairisha utekelezaji wa kitaifa wa mtaala huo. Matatizo haya ni pamoja na kutohusishwa kunakofaa kwa mtaala wenyewe na malengo ya kitaifa, walimu kutopewa mafunzo yafaayo ili kujitayarisha vilivyo, uteuzi na uundaji wa vifaa zifaazo kwa mafunzo, utahini na kutozingatia gharama ya utekelezaji wa mtaala mpya.
Maswala haya yalifanya ushirikishi wa mtaala huu kuwa mgumu pamoja na kwamba wadau wengi bado wanaamini kwamba mtaala huu mpya utaboresha mafunzo katika shule. Pamoja na haya, walimu hawakuunga mkono mtaala huu kikamilifu kwa sababu nafasi yao kama walimu ilikuwa inaonekana kulegezwa kwenye mitaala. Aidha, walimu bado hawajafunzwa njia na mbinu za kufunzia mtaala mpya, mbinju za upimaji na tathmini ili kuelekeza mfumo mzima.
Mtaala wa elimu
Kuna tetesi pia kuwa changamoto zilizoukumba mtaala huu ni kuwa taratibu zilizoundwa ili kuelekeza mtaala wenyewe zilikuwa changamano, zikipunguza ubora wa mipangilio ya masomo na nafasi ya walimu katika ufundishaji.
Huku haya yakiendelea, ripoti ya Taasisi ya kutayarisha Mitaala nchini Kenya (KICD) inaeleza kuwa ni mwalimu mmoja tu kati ya watano ambaye yuko tayari kutekeleza mtaala mpya darasani. Katika ripoti yake ya katikati ya mwaka huu inaeleza kuwa wazazi ambao watatajiriwa kuchukua nafasi muhimu katika utekelezaji wa mtaala huu wa 2-6-3-3 ambao unachukua nafasi ya mfumo wa 8-4-4, bado hawajaelezwa majukumu yao.
"Zaidi ya nusu, alimia 57, ya walimu walieleza kuwa kwa kiasi Fulani wako tayari kutekeleza mtaala mpya wa 2-6-3-3," ripoti hiyo inaeleza.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa ni asilimia 3 tu ya walimuwa mabo walieleza kuwa tayari kabisa katika kutekeleza mtaala huo huku wengine asilimia 20 wakieleza kuwa "wako tayari". Asilimia 13 ya walimu walieleza kutokuwa tayari kuutekeleza mtaala huku asilimia nyingine 7 wakieleza "kutokuwa tayari kabisa", ripoti hiyo inasema.
Mtaala huu ambao ulikuwa utekelezwe mwaka huu jambo ambalo lilihairishwa hadi mwaka ujao lakini sasa unahairishwa hadi mwaka wa 2020 kwa sababu ya kukosa kujitayarisha na mambo muhimu kutokuwa tayari wakiwemo walimu ambao hawajengewa uwezo kupitia kwa mafunzo, wazazi, vifaa vya kufunzia na mfumo wa tathmini na utahini.
Wanafunzi
Kuhusiana na utahini na mfumo mzima, ripoti hiyo ilieleza kuwa walimu hawana ufahamu kuhusiana na jinsi ya kuwatahini wanafunzi na utayarishaji wa masomo kulingana na maelekezo ya mfumo mpya.
"Ripoti hii pia yameonyesha kuwa kuna kushughulikia masuala mengi katika baadhi ya masomo. Hatua hii inawza kurudisha nyuma tendo la kuhakikisha kuwa tunalenga kufunza uwezo badala ya kuwajaza wanafunzi ufahamu tu. Hili linafaa kutosisitizwa maana mabadiliko ya sasa yanalega kuwashirikisha wanafunzi kutekeleza kupitia kwa kuonyesha ikilinganishwa na kuwajaza wanafunzi na ufahamu wa mambo mengi," ripoti inaeleza.
Ripoti hii inarandana na ripoti nyingine ambayo ilitayarishwa na Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC), ambayo pia ilitilia shaka utekelezwaji wa mtaala mpya kwa sababu ya uelewa wa chini wa masomo mbali mbali miongoni mwa waalimu wanaofaa kufundisha shuleni. Asilimia 27 ya walimu hawana uelewa wa masomo ambayo hufundisha shuleni. Kuna walimu wapatao 312,060 nchini Kenya wakifundisha shule za msingi na zile za upili.
Ripoti hii ya Tume ya Kuwaajiri Walimu Kenya (TSC) inakubaliana na nyingine ya Benki ya Dunia ambayo ilitolewa mwezi wa Aprili mwaka huu jijini Nairobi, ambayo ilionyesha kuwa walimu wa Hisabati na lugha hawangemudu kupata asilimia 100 katika kazi ya wanafunzi kwa darasa la hatua ya 4.
Walimu waliotahiniwa kuhusiana na mtaala huu kwa darasa la hatua ya 4 katika somo la Kiingereza walizoa alama za wastani za asilimia 63 huku katika Hisabati wakijizolea asilimia 77.
Changamoto ya sasa hasa katika kuhairisha utekelezwaji wa mtaala mpya ni kuhusiana na wachapishaji wa vitabu ambao watapoteza mabilioni ya pesa kwa sababu ya hatua hii huku wazazi wakiwa wamenunua vitabu vipya vya mtaala huu. Aidha, kuna wasiwasi kuhusiana na wanafunzi ambao wanatakiwa kurejelea mafunzo katika mtaala wa 8-4-4. Mambo haya yanatisha kuzua wasiwasi katika sekta ya elimu nchini Kenya yasiposhughulikiwa kwa haraka.
Itakumbukwa kuwa wafadhili na washirika wengine wa Kenya walikuwa wamepotoa pesa nyingi kufadhili taratibu nyingi katika kuanzishwa na utekelezaji wa mtaala huu hasa katika kununua nyenzo za kujifunzia. Mamilioni ya pesa yalikuwa pia yametolewa katika kutayarisha mikutano miwili ya kitaifa pamoja na kuwalipa wataalamu walioshiriki katika mchakato mzima.
waziri wa elimu nchini Kenya Amina Mohamed
Shule za kibinafsi ambazo hazijafurahishwa na hatua hii zimeeleza kutopendezwa na hatua hii kwa sababu raslimali nyingi zimetumika katika kuutayarisha mtaala mpya.
"Kuhusiana na mtaala mpya na utekekelzaji wake, maoni ya chama cha wenye shule za kibinafsi ni wazi; mbele daima, nyuma haturudi. Tuliyaanzisha haya. Ni lazima tuishi nao ili tuendelee kuurekebisha tunavyoendelea ili kuufanya bora," chama kilieleza baada ya kupokea habari za kuhairishwa kwa utekelezaji wa mtaala.
Mwenyekiti wa chama cha kitaifa cha wazazi nchini Kenya, Nicholas Maiyo alisema kuwa wazazi wa Kenya walishangazwa na hatua hiyo ya serikali.
"Tulikuwa tumejitayarisha kwa mtaala mpya kiasi cha kununua vitabu. Sasa hatujui tufanye nini," Bwana Maiyo alisema.
Vuta nikuvute hii inamaana kuwa kuna maswala yanayofaa kusghulikiwa na wadau wote watahitaji
Kilichodhahiri ni kwamba kuna maswali ambayo yanatilia shaka utekelezwaji wa mtaala mpya wa elimu katika shule za Kenya. Itabidi maswala haya kushughulikiwa kwa mapana na marefu ili kuhakikisha kuwa utekelezwaji huo utakapoanza, malengo ya mabadiliko ya mtaala yatafikiwa.
Prof. Mogambi, ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi: hmogambi @ yahoo.co.uk
Comments
Post a Comment