Mwanamuziki nyota kutoka Tanzania Diamond Platnumz amefafanua kilichotokea kati yao na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) hadi wakaruhusiwa kuondoka nchini humo kwenda Kenya kutumbuiza.
Diamond, akiandamana na mwenzake Rayvanny na Queen Darleen, amewaambia wanahabari kwamba waliiandikia serikali barua kueleza kwamba walikubali walikuwa wamekosea kuucheza wimbo wa Mwanza uliofungiwa kwenye shoo yao eneo la Mwanza mwishoni mwa wiki.
Walijitetea kwamba awali, hawakuwa wameucheza wimbo huo kwenye shoo zao.
Kadhalika, walieleza kwamba marufuku dhidi yao ingewaharibia sifa na pia kuwasababishia hasara kutokana na tamasha zao walizokuwa wameandaa kipindi hiki cha sikukuu.
“Na tukawaambia pia kwamba tuna shoo nyingine ambazo ziko Kenya, na sehemu tofauti ambazo tayari zishalipwa (tiketi zishalipiwa),” amesema Diamond.
“Kwa hivyo, tusipotumbuiza pia tutatengeneza picha mbaya, pia na hasara kwa sababu pia sisi tunafanya biashara.”
Diamond, ambaye jina lake halisi ni Nasibu Abdul Juma Issaack na Rayvanny ambaye jina lake halisi ni Raymond Shaban Mwakyusa, wamepanga shoo kadha nchini Kenya chini ya Wasafi.
Jumatatu 24 Desemba watakuwa mjini Embu, kisha watumbuize Mombasa tarehe 26 Desemba kabla ya kurejea Nairobi Mkesha wa Mwaka Mpya.
Diamond ana shoo pia visiwani Comoro mnamo 28 Desemba.
Comments
Post a Comment