Rais Kim Jong Un atangulia Singapore kumsubiri Trump

Rais Kim Jong Un Atangulia Singapore Kumsubiri Trump
Kiongozi mkuu wa Korea Kaskazini Kim Jong Un anatarajiwa kuwasili leo nchini Singapore kwa ajili ya mkutano wa kihistoria kati yake na Rais Donald Trump wa Marekani uliopangwa kufanyika Jumanne, vyombo vya habari vimesema.

Shirika la habari la Reuters lilinukuu chanzo kimoja kikisema kuwa Kim anatarajiwa kusafiri hadi katika uwanja wa ndege wa Changi, Singapore leo Jumapili.

Juhudi za Reuters kutaka kupata uhakika kutoka mamlaka za usafiri wa anga Singapore ziligonga mwamba baada ya kukataa kuzumgumzia safari hiyo ya Kim.

Kim na Trump pamoja na mambo mengine watajadili ajenda ya kuondoa silaha za nyuklia katika Rasi ya Korea na kwamba rais huyo wa Marekani anatarajiwa kumtaka Kim kuachana na uundaji wa silaha hizo.

Wakati Kim akijiandaa kuwasili leo kwa ajili ya mkutano huo wa kihistoria, viongozi wakuu wa nchi zilizoendelea zaidi kiviwanda duniani (G7) Ijumaa walianza mkutano wa siku mbili nchini Canada ambao mada kuu ni biashara duniani na Korea Kaskazini.

Mkutano huo ulifanyika Charlevoix katika jimbo la Quebec lililopo mashariki mwa Canada.

Biashara huru na uchumi wa dunia ilikuwa mada kuu katika siku ya kwanza. Mkutano huo unafuatia hatua ya Rais Donald Trump kuendelea na msimamo wake wa kulinda masoko ya ndani,ushuru wa forodha katika bidhaa za chuma cha pua na alumini uliowekwa na utawala wa Trump umeifanya Marekani kutofautiana na mataifa mengine ya G7.

Katika kikao cha jana Ijumaa, vyanzo vya habari vilisema kuwa Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe aliwaambia viongozi wenzake kuwa majibizano ya vikwazo vya kibiashara ya papo kwa papo yataathiri uchumi wa dunia kwa kiwango kikubwa na hayatamnufaisha mtu yeyote.

Comments