Mfumo wa Simba waisafishia njia Azam FC kumaliza nafasi ya pili VPL

Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Azam FC imefanikiwa kuchomoza na ushindi wa jumla ya mabao 4 – 1 dhidi ya Tanzania Prisons baada timu hiyo kubadili mfumo ‘Formation’ kwenye mchezo huo, kwa timu hiyo kutumia 3-5-2 ambao ndiyo unao tumika siku zote na Mabingwa wapya wa ligi kuu soka Tanzania Bara Simba.

Matokeo ya mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliopigwa majira ya usiku kwenye dimba la Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam yamezidi kuisafishia njia Azam FC ya kumaliza kwenye nafasi ya pili kwenye msimamo hadi sasa ikiwa inaishikilia ikifikisha pointi 55 ikiiacha Yanga iliyojikusanyia 48 huku ikiwa na mechi mbili mkononi.

Wachezaji wengine waliokuwa wagonjwa kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Nahodha Msaidizi, Agrey Moris, wakirejea kwa mara nyingine kikosini baada ya hali zao kurejea vema.

Azam FC ilidhihirisha kuwa imepania kuibuka kidedea baada ya kujipatia bao la kwanza dakika ya 17 likifungwa kiufundi na Shaaban aliyeitumia pasi nzuri ya kiungo Frank Domayo ‘Chumvi’, ambaye alionyesha uelewano mzuri katikati mwa uwanja akiwa na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Nahodha Himid Mao ‘Ninja’.

Domayo akaendeleza ubora wake kwa kuifungia bao la pili Azam FC dakika ya 22 akitupia kwa shuti la mbali lililomshinda kipa wa Prisons, Moses Matulanga, pasi safi akiipata kutoka kwa beki wa kushoto, Bruce Kangwa.

Shaaban alirejea tena wavuni dakika ya 31 akiindikia bao la tatu Azam FC akimtesa kipa kwa shuti la kukunja ‘curve’ baada ya kupokea pande kutoka kwa Sure Boy, ambaye aliweka uhai eneo la kati la timu yake kwa kuisambaratisha Prisons akishirikiana na viungo wenzake.

Wakati watu wakitarajia mpira ungeenda mapumziko kwa matokeo hayo, Shaaban alikamilisha hat-trick yake kwa kuipatia Azam FC bao la nne akitumia vema pasi ya juu ‘outer’ iliyopigwa na Domayo. Hiyo ni hat-trick ya kwanza kwa Shaaban kwenye ligi tokea apandishwe timu kubwa msimu uliopita.

Aidha hat-trick hiyo inamfanya Shabaan kufikisha jumla ya mabao nane kwenye ligi msimu huu akiwa ndio mfungaji kinara wa Azam FC huku akijiwekea rekodi ya kufunga mabao sita ndani ya mechi nne mfululizo zilizopita za ligi.

Prisons ilijitutumua na kupata la kufuatia machozi dakika ya 70 lililofungwa kwa mkwaju wa penalti na mshambuliaji wao hatari, Mohamed Rashid na kufanya mpira kumalizika kwa ushindi huo mnono wa Azam FC.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kupumzika leo siku ya Jumatatu kabla ya kurejea mazoezini Jumanne jioni kuanza maandalizi ya kufunga pazia la ligi kwa kumenyana na Yanga Mei 28 mwaka huu, utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kikosi cha Azam FC

Razak Abalora, Abdul Omary, Bruce Kangwa, David Mwantika, Agrey Moris, Abdallah Kheri, Himid Mao (C), Frank Domayo, Salum Abubakar/Joseph Mahundi dk 87, Shaaban Idd/Mbaraka Yusuph dk 76, Yahya Zayd/Enock Atta dk 76.

Comments