Kuna fitna nyingi nawekewa kwa kuwa mimi sio Mtanzania – Christian Bella

Msanii wa muziki, Christian Bella amedai kuna mazingira ya kunyimwa fursa ambayo yamekuwa yakimtokea kwa kuwa yeye sio Mtanzania.
Muimbaji huyo ambaye ni raia wa Congo, amedai kama angekuwa ni Mtanzania kwa kazi za muziki alizofanya ikiwemo Nani Kama Mama tayari angekuwa ameshapewa hata tuzo za muziki.

“Ni akili ya ziada ambayo Mungu amenipa na heshima ya jinsi ya kuishi, unajua kazi yetu ina mambo mengi, ina fitna, hakuna mtu anaweza kupenda wewe uwe mbele ukizingatia mimi sio Mtanzania, kuna vikwazo vingi wananiwekea, ukiweka hivi wanakubana hapa,” Bella alimwambia DJ Hazuu wa Radio 5 Arusha.

Aliongeza, “Yaani namaanisha kama ningekuwa Mtanzania ningekuwa mbali zaidi, kwa sababu sio kwamba sipendwi napendwa sana na mashabiki mpaka na viongozi wa serikali, lakini nadhani kama ningekuwa Mtanzania kuna vitu vingi zaidi ningefanya au ningekuwa mbali zaidi,”

Muimbaji huyo amedai ‘Nani Kama Mama’ ni wimbo ambao ulitakiwa upewe tuzo lakini waliwepewa watu wengine wenye nyimbo za kawaida kwa madai yeye sio Mtanzania.


Comments