Mwigizaji filamu maarufu nchini Tanzania, Elizabeth Michael anayefahamika pia kama Lulu amebadilishwa kifungo na sasa atatumikia adhabu hiyo akiwa nje yaani 'kifungo cha nje'.
Mcheza filamu huyo ni miongoni mwa waliofaidi kutokana na msamaha wa Rais.
Lulu alihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela Novemba mwaka jana baada ya kupatikana na hatia ya kumuua bila kukusudia msanii mwenzake Steven Kanumba.
Idara ya Magereza nchini Tanzania kupitia taarifa imesema Lulu amebadilishiwa adhabu kwa amri ya Mahakama Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam.
Taarifa ya idara hiyo imesema mfungwa huyo aliachiliwa kutoka gerezani "kutokana na kukidhi vigezo vya kisheria na kuonesha tabia njema akiwa gerezani".
Lulu alikuwa amefungwa gereza la Segerea, Dar es Salaam mnamo 13 Novemba 2017 baada ya kuhukumiwa.
Idara ya magereza imesema kwa mujibu wa Sheria ya Magereza mfungwa yeyote (isipokuwa mfungwa wa kunyongwa na wa maisha) mara baada ya kuppkelewa gerezani na hupata msamaha wa theluthi moja ya kifungo chake.
"Hivyo, mfungwa nambari 1086/2017 Elizabeth Michael maarufu kwa jina la Lulu alipata msamaha huo na alitakiwa kuachiliwa tarehe 12 Machi, 2019," taarifa hiyo imesema.
Mnamo 26 Aprili, wakati wa kuadhimisha Siku ya Muungano, Rais wa Tanzania John Magufuli kwa kutumia madaraka aliyopewa na katiba alitoa msamaha wa robo moja ya adhabu kwa wafungwa wote waliokuwa na sifa za kunufaika na msamaha.
"Kufuatia msamaha huo, ... Lulu naye alinufaika na msamaha huo na hivyo basi kutakiwa kutoka gerezani tarehe 12 Novemba, 2018," taarifa ya magereza inasema.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa Sheria ya Huduma kwa Jamii ya mwaka 2002 inaruhusu wafungwa ambao vifungo vyao havizidi miaka mitatu kunufaika na utaratibu ambao humpa mfungwa fursa ya kutumikia kifungo chake nje ya gereza na kufanya shughuli au kazi zisizo na malipo kwa manufaa ya jamii.
Comments
Post a Comment