Bosi wa Tip Top Connection, Hamis Taletale maarufu Babu Tale, umerudishwa rumande mchana huu (Mei 23, 2018) na atakaa huko kwa muda usiojulikana mpaka Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda Maalum, Wilbard Mashauri aliyetoa amri ya kumatwa atakapo rejea ofisini baada ya kupata dharula ya kikazi.
Awali amri hiyo pia, ilielekeza atakapokamatwa meneja huyo wa Diamond, ilitaka apelekwe Gereza la Ukonga akiwa ni mfungwa wa kesi ya madai, hadi hapo mahakama hiyo itakapotoa maelekezo mengine.
Baada ya kufikishwa Mahakama Kuu Jumatano hii, alikutana na Naibu Msajili, Ruth Massam na kutoa muda wa dakika kumi kwa upande wa Sheikh Mbonde na upande wa Babu Tale wazungumze na kuangalia kama kuna namna wanaweza kumalizana wenyewe.
Wawili hao walishindwana kuelewana na ndipo msajili huyo alivyotoa amri ya Tabu Tale kurudishwa rumande hadi pale Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda Maalum, Wilbard Mashauri atakapo rejea kazini.
Katika kesi ya msingi, Sheikh Mbonde alikuwa akidai kuwa aliingia mkataba na kampuni ya kina Babu Tale (Tiptop Connection) ili wamrekodi mahubiri yake kisha wayauze na kugawana mapato.
Hata hivyo baada ya kurekodi masomo saba, walimkatia mawasiliano na alipowatafuta na kukutana nao wakamweleza kuwa wameamua kuachana na mpango huo.
Sheikh Mbonde alidai kuwa akiwa kwenye mahubiri Dodoma ndipo akakutana na mikanda ya video katika mfumo wa DVD yenye mahubiri yake huku kukiwa na namba za simu za viongozi hao wa Tiptop.
Sheikh Mbonde alidai baada ya kufanya uchunguzi alibaini kuwa DVD hizo zilikuwa zikiuzwa katika mikoa mbalimbali, ndipo akawafungulia kesi ya madai ya fidia kutokana ukiukwaji wa Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki.
Baada ya kupeleka madai yake Mahakamani, Mahakama ilimuamuru Babu Tale kumlipa Mhadhiri wa Dini ya Kiislamu, Sheikh Hashim Mbonde kiasi cha Sh250 milioni, baada ya kupatikana na makosa ya ukiukwaji wa haki za hakimiliki kwa kutumia masomo yake kibiashara bila ridhaa yake kinyume cha Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki.
Comments
Post a Comment