Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe (wa pili kulia) akikabidhi rasmi bendera kwa Nahodha wa timu ya Azania, Khalid Sultan Said. Wanaoshuhudia tukio hilo ni Mjumbe wa Bodi ya Standard Chartered Tanzania, Ami Mpungwe (suti nyeusi) na Balozi wa Uingereza nchini, Sarah Cooke (kulia).
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe ameikabidhi bendera timu ya Azania ambayo inaelekea nchini Uingereza kushiriki mashindano ya Standard Chartered Safari kwenda Anfield.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi bendera pamoja na hati za kusafiria, Waziri Mwakyembe alisema ni fursa ya kipekee ambayo Tanzania imeipata kushiriki mashindano kama hayo na ni muda sasa dunia kujua kuwa Tanzania kuna vipaji vya soka hivyo wahakikishe wanarudi nchini na kikombe."Mtuwakilishe vyema huko muendako ni muda sasa wa dunia kuwa Tanzania tuna uwezo wa kisoka, kila mmoja acheze vizuri na kuonyesha uwezo wake, tunaamini mtarudi na kikombe na nawatakia kila la kheri," alisema Waziri Mwakyembe.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi bendera pamoja na hati za kusafiria kwa timu ya Azania ambayo inaelekea nchini Uingereza kushiriki mashindano ya Standard Chartered Safari kwenda Anfield iliyofanyika katika hoteli ya Southern Sun jijini Dar Es Salaam.
Nae Mjumbe wa Bodi ya Standard Chartered Tanzania, Ami Mpungwe amesema benki yao inajivunia kupata wawaklishi kutoka Tanzania na wamesimamia gharama zote za safari kwa muda wote ambao timu itakuwa Uingereza na ni matumaini yao kuwa timu hiyo ya Azania itarejea nchini na kikombe.
"Tupo hapa kuiaga timu ya Azania ambao ni mabingwa wa Tanzania na Afrika Mashariki wa kombe la Standard Chartered Safari kwenda Anfield, tunajivunia timu hii sababu imetuletea heshima kubwa, tunawaombe ushindi mkubwa na tunategemea watakuja na ubingwa," alisema Mpungwe.
Balozi wa Uingereza nchini, Sarah Cooke akitoa pongezi kwa timu ya Azania kupata nafasi ya kwenda Uingereza wakati wa hafla ya kukabidhi bendera kwa timu hiyo inayokwea pipa kesho 18 Mei. Kushoto ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe.
Kwa upande wa Balozi wa Uingereza nchini, Sarah Cooke aliipongeza timu ya Azania kwa kupata nafasi ya kwenda Uingereza kucheza kwenye moja ya kiwanja maarufu cha Anfield lakini pia kuipongeza benki ya Standard Chartered kwa kufikisha miaka 100 tangu kuanza kutoa huduma nchini.
"Hii ndiyo nguvu ya michezo inauwezo wa kuwaunganisha watu pamoja, mnakwenda Uingereza tunaijua ni timu kubwa nawapongeza Azania kwa kupata nafasi, hongereni sana nawatakia kila la kheri najua mtafurahi kwa kipindi ambacho mtakuwa kule,
"Mnakwenda kwenye moja ya uwanja maarufu nchini Uingereza, Liverpool ni timu yenye historia na wachezaji wakubwa kama Steven Gerarld, Kenny Dalglish na wengine wengi, pia niwapongeze Standard Chartered kwa kufikisha miaka 100 tangu kuanza kufanya kazi Tanzania," alisema Cooke.
Naye nahodha wa timu hiyo, Khalid Sultan Said aliahidi kuwa timu hiyo inajiamini kuwa inauwepo wa kupambana na timu zingine na kuahidi kuwa itahakikisha kikombe kinakuja nchini.
Timu hiyo itaondoka nchini Mei, 18 watafika Mei, 19 wakiwa huko watakutana na timu zingine, Mei, 20 watatembelea uwanja wa Anfield, Mei, 21 watashuhudia mchezo wa Liverpool na Middlesbrough na baada ya hapo wataingia uwanjani kwa ajili ya mashindano na watarejea nchini Mei, 22.
Comments
Post a Comment