WADUDU WATUMIKA KUPIMA UBORA WA MAJI MTONI

bbc
Wanakijiji wa kijiji cha Mngeta wakiangalia wadudu wanatumika kutathimini ubora wa maji ya mto

Nchini Tanzania, katika mkoa wa Morogoro, wilaya ya Kilombero, baadhi ya wanakijiji cha Mngeta wameanza kunufaika na mafunzo maalumu ya kutathimini ubora wa mito kwa kutumia viumbe hai, hasa wadudu wasio na uti wa mgongo.
Watafiti wamebaini kwamba, teknolojia ijulikayo kama miniSASS ndio njia nyepesi inayoweza kutumiwa na mtu mwenye kiwango chochote cha elimu na kwa gharama nafuu ikilinganishwa na utafiti wa maabara, hivyo inaweza kusaidia jumuia za watumia maji kujua ni kwa kiwango gani vyanzo vya maji vimeathirika kutokana na shughuli za binadamu kama vile ukulima wa pembezoni mwa mto na shughuli nyengine kama vile kufua na kuchota mchanga.

bbc
Dk. Lulu Kaaya mwenye fulana nyeupe ambae ni mtafiti wa sayansi za maji kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, akitoa maelekezo kwa wanakijiji

Mafunzo hayo yakiongozwa na Dk. Lulu Kaaya ambae ni mtafiti wa sayansi za maji kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, chini ya udhamini wa Shirika la Wanyamapori wakishirikiana na IUCN SUSTAIN, umejumuisha wanakijiji takriban 30 ambao ni watumia maji ya mto Mchombe.
"Tunatumia wadudu kuonyesha hali ya ubora wa mto. Kwa mfano, kunapotokea uharibifu wa mto, labda kumwagwa kwa kemikali kwenye mto, wapo wadudu ambao wataishi kwenye mto na wapo ambao hawataweza kuvumilia kemikali na kuna watakaokufa. Kile kiasi cha waliovumilia ndio kinakupa mwanga wa kuweza kubaini kulitokea nini, na kiasi cha uharibifu uliofanyika," anaeleza Dk. Lulu Kaaya.

bbc
Wanakijijini na mtaalamu wa wakichagua wadudu wa kutumia katika utafiti

Kwa mujibu wa Damas Patrick Mmbaga, ambae ni mtaalamu wa maji kutoka Shirika la Wanyamapori Afrika, teknolojia hii rahisi inatoka Afrika Kusini na inaweza kutumiwa na mtu yoyote bila kujali kiwango cha elimu alichonacho.
"Tunawafundisha jinsi ya kufanya tathmini ya mto. Wakishatathmini ubora wa mto, watapata majibu na watajua mto uko katika hali gani. Kama mto umeharibiwa watajua kwa nini, labda kuna watu wanalima katika kinga za maji, au kuna ng'ombe au watu wanatoa mchanga," ameongeza kusema Damas.
Vifaa vinavyotumika kufanya utafiti huo, ni pamoja na nyavu za kuvulia kwa ajili ya kukamatia wadudu, sinia za plastiki rangi nyeupe, na makabrasha yenye taarifa zinawasaidia kulinganisha sifa za wadudu ili kuwaweka katika makundi maalumu. Miongoni mwa wadudu wanaotumiwa ni konokono, kaa, luba, kamba na wengineo ambao hawana utii wa mgongo.

bbc
Dk. Lulu Kaaya ambae ni mtaalamu wa utafiti akitoa maelekezo kwa wanakijiji wa kijiji cha Mngeta

Baada kukusanywa kwa wadudu na kufanyiwa tathmini, ndipo wanakijiji wanapobaini iwapo maji ya mto umeathirika kutokana na shughuli za binadamu au la, na hatimae kujua hatua gani za kuchukua.
Tanzania licha ya kuwa na vyanzo vingi vya maji, lakini baadhi ya vyanzo hivyo viko hatarini kutokana na shughuli za binadamu zinazoendelea pembezoni, kama vile kulima, kulisha mifugo na hata kuchota mchanga hivyo kusababisha mmomonyoko.
Ingawa kuna sheria inazuia matumizi mabaya ya vyanzo vya maji, lakini kila kukicha, kasi ya uharibifu inaarifiwa kuongezeka

Comments