UPINZANI KUTANGAZA MGOMBEA WAKE KENYA

Viongozi watano wa muungano wa upinzani Kenya (NASA)
Viongozi watano wa muungano wa upinzani Kenya (NASA)

Muungano wa vyama vya upinzani nchini Kenya unatarajiwa kumtaja atakayewania urais dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta kwenye uchaguzi mkuu wa mwezi Agosti.
Tangazo hilo litafanyika huku nchi hiyo ikimaliza shughuli kura za mchujo za vyama, ambazo zimekumbwa na vurugu na madai ya kuiba kura.
Huku zikiwa zimesalia siku 102 tu kabla ya uchaguzi, muungano mkuu wa upinzani Kenya ulikuwa na muda mdogo kumtaja kiongozi wao. Muungano huo wa National Super Alliance, yaani NASA, una wanaume watano wote wanaotaka kuongoza, lakini inatarajiwa kuwa jopo litamchagua Raila Odinga.
Vigogo wengine kwenye muungano huo ni makamu wa rais wa zamani Kalonzo Musyoka, makamu wa rais wa zamani Musalia Mudavadi, waziri wa zamani wa mambo ya nje Moses Wetangula na mwenyekiti wa zamani wa baraza la magavana Isaac Ruto.
Bw Ruto, anayeongoza chama cha Chama cha Mashinani (CCM) alikuwa kwenye muungano wa vyama vinavyomuunga mkono Bw Kenyatta kabla ya kuhama na kuunda chama chake.
Bw Odinga ndiye kiongozi wa chama cha ODM, ambacho kina wabunge wengi zaidi katika Bunge la sasa.
 
Iwapo atachaguliwa kuwa mwaniaji wa NASA, basi itakuwa ni mara ya nne kwake yeye kupigania urais.
Kiongozi huyo bado anasisitiza kuwa alishinda uchaguzi wa mwaka 2007 ambapo rais wakati huo, Mwai Kibaki alitangazwa mshindi, na kuzua tafrani nchini Kenya ambapo watu zaidi ya elfu moja waliuawa.
Huku hayo yakijiri, wanasiasa wengi wanaendelea kupoteza viti vyao kwenye kura za mchujo.

Bw Musyoka, Bw Odinga na Bw Wetangula
Bw Musyoka, Bw Odinga na Bw Wetangula

Wakenya kwenye mtandano wamekuwa wakiendesha kampeni inayoitwa Opresheni Fagia Wote, na mwandishi wetu Ferdinand Omondi anaripoti anasema huenda wanafanikiwa.
Baadhi ya maeneo ya uchaguzi yamemfuta kazi Gavana, Seneta, wabunge na madiwani wote.
Kampeni ya Fagia Wote inapania kuonyesha ghadhabu ya Wakenya kwa jinsi taifa hilo limeendeshwa kwa miaka minne iliyopita. Kumezuka vurugu kwenye sehemu kadhaa nchini na pia madai ya kuiba na kununua kura.
 
Askofu mmoja wa kike, Margaret Wanjiru ambaye amewahi kuwa waziri, ambaye kwa sasa alikuwa anawania kuwa Gavana mpya wa Nairobi, alilala kwenye seli ya Polisi alipokamatwa jana kwa madai ya kuzua rabsha katika kituo cha uchaguzi.
Kura za mchujo zinafaa kumalizika Jumapili.
Uchaguzi mkuu utafanyika tarehe 8 Agosti.

Comments