Mwanamke mmoja wa Ufaransa ''amefufuliwa'' na afisa mmoja wa polisi ambaye alimfanyia matibabu ya dharura kwa jina CPR saa moja baada ya maafisa wa afya kusema kwamba amefariki.
Mwanamke huyo ambaye hakutajwa jina na ambaye amekuwa akiugua ukosefu wa hamu ya kula alipatikana amezirai akiwa na mwanawe wa miaka 18 baada ya kukabiliwa na kiharusi.Maafisa wa afya walifika nyumbani kwake mjini Paris lakini walishindwa kumsaidia mama huyo mwenye umri wa miaka 49.
Lakini maafisa wa polisi walioitwa ili kuandika ripoti walihisi uhai ndani ya tumbo lake.
Taarifa ya gazeti la Le Parisien imesema kuwa maafisa hao wa afya walikuwa wamesema kuwa amefariki na kutia saini cheti chake cha kufariki.
Lakini maafisa hao wa polisi waliowasili saa moja baadaye walihisi uhai katika tumbo lake walipoondoa nguo aliyokuwa amefinikwa nayo.
Wakati afisa mmoja alipoangalia mishipa yake walibaini kwamba moyo wake ulikuwa ukipiga.
Huku afisa mmoja akimshika mkono wake na kuzungumza naye mwengine alipiga simu katika idara ya zima moto ili kuchukua maelezo ya kumfufua.
Baadaya ya dakika 30 za jaribio la kumfufua ,mwanamke huyo aliyedhaniwa kufariki alianza tena kupumua.
Comments
Post a Comment