MAREKANI: IRAN INAFANYA UCHOKOZI WA HALI YA JUU

Rex Tillerson. Picha: 19 April 2017
Rex Tillerson amesema Iran imeendelea kuwa "mfadhili wa ugaidi"
 
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson ameituhumu Iran kwa kufanya "uchokozi wa hali ya juu" unaoendelea ambao amesema unanuia kuvuruga uthabiti katika Mashariki ya Kati na kuhujumu juhudi za Marekani katika kanda hiyo.
"Iran isipochukuliwa hatua inaweza kwenda njia sawa na ya Korea Kaskazini na kuubeba ulimwengu wote katika safari hiyo," Bw Tillerson amesema.
Rais Donald Trump tayari ameagiza utathmini mpya ufanywe kuhusu mkataba uliotiwa saini kati ya nchi za Magharibi kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.
Hata hivyo, Marekani imekiri kwamba Tehran inatii makubaliano hayo ya mwaka 2015.

Iran kufikia sasa haijasema lolote kuhusu tamko hilo jipya kutoka kwa Marekani.
Iran imekanusha mara kwa mara tuhuma kutoka kwa nchi za Magharibi kwamba inajaribu kustawisha silaha za nyuklia.
Jumanne, Marekani iliituhumu Korea Kaskazini na kusema taifa hilo lilikuwa linajaribu kufanya "uchokozi kutokee jambo fulani", baada ya nchi hiyo kufanya jaribio la kombora ambalo lilifeli mwishoni mwa wiki.
Kuijibu Marekani, Korea Kaskazini ilisema inaweza kuwa ikifanya majaribio ya makombora kila wiki.
Aidha, ilionya kwamba itaikabili Marekani kwa vita vikali iwapo taifa hilo litathubutu kuishambulia kijeshi.

'Vitisho vingi'

Jumatano, Bw Tillerson alsiema utathmini huo mpya kuhusu Iran, ambao aliutangaza katika Bungela Congress siku moja awali, kando na kutathmini iwapo Tehran imetimiza makubaliano ya mkataba huo wa nyuklia pia utachunguza vitendo vya Iran Mashariki ya Kati.

Bw Tillerson aliituhumu Iran kwa kuhujumu juhudi za Marekani nchini Lebanon, Iraq, Syria na Yemen.
"Mpango wa kina wa sera kuhusu Iran unatuhitaji tuangazie vitisho hivi vinavyoletwa na Iran, na ni wazi kwamba ni vingi (vitisho)," alisema.
Tehran
Bw Tillerson awali alikiri kwamba Iran ilikuwa imeheshimu makubaliano ya mkataba huo wa 2015, lakini aliibua wasiwasi kuhusu taifa hilo akisema limeendelea kuwa "mfadhili wa ugaidi".
Rais Trump kwa muda mrefu amekuwa akisema mkataba huo kuhusu Iran "ndio mbaya zaidi kuwahi kutiwa saini".
Hata hivyo, mtangulizi wake Barack Obama alisema mkataba huo, kati ya Iran na mataifa sita yenye ushawishi duniani zikiwemo China, urusi na Uingereza, ilikuwa ndiyo njia bora zaidi ya kuizuia Iran kustawisha silaha za nyuklia.

Comments