MAAFISA WA UN WALIOTEKWA DRC WAACHILIWA HURU

Wanajeshi wa Riek Machar
Wapiganaji wengi watiifu kwa Riek Machar walikimbilia DR Congo

Maafisa wa Umoja wa Mataifa wanasema wafanyikazi 16 waliokuwa wametekwa na kuzuiliwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wameachiliwa huru bila kujeruhiwa.
Watu hao walikuwa wametekwa nyara katika kambi moja iliyopo jimbo la Kivu Kaskazini na kundi la waasi mia moja kutoka Sudan Kusini, ambao walitaka kuhamishwa hadi nchi nyingine.
Waasi hao ambao hawakuwa na silaha ni miongoni mwa mamia ya wafuasi wa aliyekuwa makamu wa rais wa Sudan Kusini, Riek Machar.
Walihamishwa hadi kambi ya Munigi kaskazini mwa Goma Agosti mwaka uliopita
Waandishi wa habari wanasema raia wa DRC wanaoishi Kivu Kaskazini wana wasiwasi kuhusu kuwepo kwa waasi hao wa Sudan Kusini, na wanahofia kuwa wanaweza kusababisha kudorora kwa usalama katika eneo hilo.
Waasi 530 wa zamani kutoka Sudan Kusini wanaishi katika kambi ya Munigi, nje ya Goma, ambako walikimbilia wakati mapigano yalizuka mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba.

"Tunafurahia kuthibitisha kwamba wafanyakazi wote 16 wa MONUSCO, ambao walikuwa wamewekwa katika kambi ya wapiganaji wa zamani huko Munigi, wameachiliwa," alisema afisa mmoja wa Umoja wa Mataifa.
Watu hao 16 walifanya kazi kwa lengo la Umoja wa Mataifa, unaojulikana kama MONUSCO, lakini hakuna taarifa kuhusu uraia wao. .
"Wafanyakazi wote wamerudi makwao wakiwa salama, "alisema afisa huyo.
Wapiganaji hao ambao walinyang'anywa silaha kabla ya kuingia kambini wamekuwa wakidai kuhamishwa kwa miezi kadhaa, lakini maafisa wa Umoja wa Mataifa hawajaweza kupata nchi zilizo tayari kuwachukua watu hao.
Kiongozi wa waasi Riek Machar bado yupo nchini Afrika Kusini na amezuiwa asirudi Sudan Kusini.
Baada ya kupata uhuru kutoka Sudan mwaka 2011, Sudan Kusini ilitumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe Desemba mwaka 2013. Watu karibu 3.5 milioni wamelazimika kukimbia makwao.

Comments