WAZIRI MKUU AONYA KUHUSU VITA YA MADIWANI NA WATUMISHI

Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa amewataka wakuu wa idara kwenye Halmashauri za wilaya na manispaa wasaidie kutoa utaalamu badala ya kupingana na madiwani ili wawezeshe kuleta maendeleo kwa wananchi.

Ametoa wito huo Alhamisi hii wakati akizungumza na watumishi mbalimbali wa Halmashauri ya wilaya ya Mabada na viongozi na watendaji wa mkoa wa Ruvuma akiwa katika siku ya pili ya ziara yake mkoani humo.

“Wakuu wa idara nyie ni washauri. Tumieni taaluma zenu kutoa ushauri, semeni bila woga pale inapodidi. Ninawasihi waheshimiwa madiwani wasitumie fursa yao ya ‘kuazimia’ pale inapotokea kuna watumishi wenye msimamo,” alisema Majaliwa.

Akizungumzia kuhusu ukusanyaji wa mapato, Waziri Mkuu amesema serikali iko makini kwenye matumizi kwa kila senti inayokusanywa na akawataka watumishi hao kila mmoja aongeze mapato ya serikali kupitia sekta aliyopo. Pia amepiga marufuku matumizi holela ya fedha za umma.

“Kuanzia leo, marufuku kwa fedha iliyokusanya kwa mapato ya ndani kutumika bila utaratibu. Serikali hii haina mzaha na miradi inayotekelezwa chini ya viwango. Mtumishi ukiharibu hapa Madaba, usidhani utahamishwa, tunamalizana na wewe hapahapa. Wala usiombe ndugu yako akuombee uhamisho, tutakufuata hukohuko,” alisisitiza.

Comments