Jeshi la polisi mkoani Dodoma, linawashikilia askari watatu wa wanyamapori wa pori la akiba Swagaswaga wilayani Kondoa, wakituhumiwa kumuua mkazi wa kijiji cha Olimba wilaya ya Chemba kwa kumpiga risasi mgongoni wakimtuhumu kubeba nyama pori.
.
Akizungumza ofisini kwake leo, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Lazaro Mambosasa, alisema tukio hilo lilitokea Disemba 31,mwaka jana saa 7:30 mchana katika kijiji cha Selya kata ya Selya wilayani humo.
“Marehemu ambaye hakufahamika jina lake lakini mkazi wa kijiji hicho, alikuwa akiendesha pikipiki huku akiwa amepakia kiroba kilichokuwa na sukari guru ndani yake, lakini askari wanyamapori hao walimhisi amebeba nyama pori na bila kumsimamisha na kumhoji waliamua kutumia bunduki zao kumuua papo hapo,” alisema Kamanda Mambosasa.
Aidha Kamanda huyo amesema baada ya kufanya mauaji hayo, askari hao waliubeba mwili huo kwenye gari walilokuwa nalo pamoja na pikipiki ya marehemu na kiroba cha sukari guru, kisha kwenda kuutelekeza mwili huo ndani ya pori hilo la Swagaswaga.
“Baada ya kuutelekeza mwili huo ndani ya pori hilo, walichukua pia pikipiki na kiroba na kuvificha kila kimoja mahali pake kwa lengo la kupoteza ushahidi wa tukio hilo”.
Kamanda Mambosasa alisema wakati askari hao wanafanya tukio hilo, walishuhudiwa na mwananchi mmoja wa kijiji hicho ambaye alijificha porini ambaye aliamua kutoa taarifa kituo cha polisi Kondoa.
Wahusika wa tukio hilo ni wanaendelea kuhojiwa kabla ya kufikishwa mahakamani ni George Grefee (26), Chini Paulo (40) na Christopher Waunko (36).
BY: EMMY MWAIPOPO
Comments
Post a Comment