KUMBE AISHA MADINDA KAUAWA

 
Marehemu Mwanaisha Mohamed Mbegu ‘Aisha Madinda’enzi za uhai wake.


Stori:waandishi wetu MENGINE yameibuka! Kifo cha aliyekuwa mnenguaji wa Bendi ya The African Stars ‘Twanga Pepeta’, Mwanaisha Mohamed Mbegu ‘Aisha Madinda’ kimeibua mengine ambapo baadhi ya watu wa karibu wanaamini kimetokana na kudungwa sindano tano za majimaji yenye madawa ya kulevya, ‘unga’ na rafiki yake, Ijumaa ‘Kubwa’ linakupa zaidi.
Kwa mujibu wa chanzo chetu makini, Aisha alidungwa kwa makusudi sindano hizo na rafiki yake mmoja ambaye polisi bado wanamtafuta, ikidaiwa lengo lilikuwa kummaliza.
YALIYOSEMWA
Akizungumza kwenye msiba wa mnenguaji huyo nyota nyumbani kulikokuwa na kilio, Kigamboni jijini Dar, mwombolezaji mmoja ambaye ni mtu wa karibu na marehemu alisema:
“Unajua siku za karibuni, Aisha alirudia kubwia unga kama zamani, sasa majuzi mimi nilikutana naye akasema yuko kwa rafiki yake, Mwananyamala (Dar), lakini huyo rafiki aliyenitajia ni mmbwia unga mkubwa na amekuwa akiwadunga sindano wenzake.
 
 Mtoto wa marehemu Aisha, Naomi akiwa katika majonzi.
“Sasa si unajua kwamba, sindano zile ukidungwa bila kipimo ni sumu mwilini. Uwezekano ni mkubwa kwamba, sindano alizodungwa na mwenzake ndizo zimechukua uhai wake,” kilidai chanzo hicho.
CHANZO KINGINE
Kwa mujibu wa chanzo kingine msibani hapo, upo wasiwasi kwamba tangu Aisha arejee Bongo akitokea Dubai kuna mtu amekuwa akimtishia maisha kwamba atamtoa roho.
Chanzo hicho kilidai kwamba, staa huyo ambaye alirudi akiwa vizuri amekuwa akipewa vitisho na mtu huyo bila kutaja sababu.
SIKU YA KIFO
Siku ya tukio, juzi Jumatano, habari zinadai kwamba, Mkurugenzi wa Vipindi wa Radio Clouds FM, Ruge Mutahaba alipigiwa simu na daktari mmoja wa Hospitali ya Mkoa wa Kitabibu Kinondoni, Mwananyamala na kuambiwa kuwa, kuna mwili wa mtu anayefanana na Aisha Madinda umetelekezwa hospitalini hapo na watu wasiojulikana na wameondoka.
Baada ya taarifa hizo, Ruge alimwendea hewani Bosi wa Bendi ya Twanga Pepeta, Asha Baraka na kumjulisha madai ya daktari.
  
Mkurugenzi wa Bendi ya The African Stars ‘Twanga Pepeta’Asha Baraka.
“Asha Baraka alikuwa Kigoma. Kwa hiyo alipopewa taarifa hizo alimpigia simu kiongozi wa wanamuziki wa Twanga Pepeta, Luiza Nyoni Mbutu na kumpa maelekezo kwamba afuatilie habari alizoambiwa na Ruge kama ni kweli.”

AISHA MADINDA NDANI YA MOCHWARI
Ikazidi kudaiwa kuwa, Luiza na wanamuziki wenzake, Lilian Tungaraza ‘Lilian Intaneti’ na Maria Soloma walifunga safari hadi Mwananyamala na kuukuta mwili wa Aisha ukiwa tayari mochwari, wakamjulisha Asha ambaye  alifunga safari na machozi juu kurejea Dar.
MTOTO WA MAREHEMU, ANAITWA NAOMI
Akizungumza na gazeti hili ndani ya Hospitali ya Mwananyamala muda mfupi baada ya mwili wa mama yake kuingizwa mochwari, binti wa Aisha, Naomi  huku akimwaga machozi, alisema:
“Mama alikuwa akiishi Kigamboni siku za karibuni. Mimi pia nikaamua kwenda kuishi naye.”
Akaendelea: “Kuna kama siku tatu nyuma mama hakuwa akilala nyumbani, jana (Jumanne sasa), asubuhi mama alinitumia meseji akisema anaomba nimtumie pesa, nikamtumia.
“Lakini leo (juzi, Jumatano) mchanamchana nilisema nimpigie simu mama nimuulize huko aliko anaendeleaje? Kabla sijafanya hivyo, mama mkubwa alinitumia meseji na kuniambia mama amefariki dunia, ndiyo nikaja huku.”
   
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Bongo Movie Unity, Steven Mengere 'Steve Nyerere' (kulia) na Luiza Mbutu (katikati) wakihesabu michango iliyopokelewa kwa njia ya simu katika Hospitali ya Mwanayamala jijini Dar es Salaam. Kushoto ni mnenguaji wa kitambo, Lilian Intanet.
KIKAO CHA FAMILIA AELEZEA KIFO CHAKE!
Binti huyo aliendelea kusema kuwa, siku za karibu, marehemu aliwahi kuwaita ndugu zake na kuwapa ujumbe wa ajabu.
“Kuna siku aliwaita ndugu zake nyumbani akasema katika familia yetu wote, mimi ndiyo nitakayeanza kufa. Sijui mama alijua atakufa ndiyo maana akasema vile,” alisema binti huyo.
MASWALI YA MSINGI
Mpaka sasa maswali ambayo yalitawala msibani ni haya! Je, ni nani aliyeufikisha mwili wa marehemu Hospitali ya Mwananyamala na kuutelekeza? Je, dokta alijuaje kuwa alikuwa Aisha Madinda?
Je, mwili wake ulipelekwa hospitalini hapo na mtu mmoja au wengi? Walitumia usafiri gani? Bajaj au teksi? Ni vyema pia polisi wa Wilaya ya Kinondoni jijini Dar wakafuatilia kifo hiki kwa undani.
Inna lillah, wainna ilaih rajiuun!




Comments