MKE WA MUIMBAJI MAARUFU BONGO AFANYIWA KITU MBAYA NA MUMEWE

Mke wa mkongwe wa Nyimbo za Injili Bongo, Rev. Cosmas Chidumule aliyejitambulisha kwa jina la Cesilia Maiko na wanaye, wanadai kutelekezwa na staa huyo huku mama huyo akiandamwa na maradhi ya kisukari.

Mke wa mkongwe wa Nyimbo za Injili Bongo, Rev. Cosmas Chidumule anayetambulika kwa jina la Cesilia Maiko.
 Kwa mujibu wa chanzo makini ambacho ni jirani wa familia hiyo, Chidumule aliyewahi kutamba na Wimbo wa Yesu ni Bwana, alidaiwa kutoweka nyumbani kwake kwa muda mrefu hivyo kuiacha familia kwenye maisha magumu na wakati mwingine kukosa hata chakula.


Baada ya kuzinyaka habari hizo, mwanahabari wetu alifika nyumbani kwa Chidumule maeneo ya Kinondoni B, Dar, mwanzoni mwa wiki hii ambapo alishuhudia hali halisi ya nyumbani hapo na hakumkuta Chidumule ila alifanikiwa kuzungumza na mkewe.

Akizungumza kwa huzuni huku akibubujikwa na machozi, mke wa Chidumule, Cesilia alisema wameishi kama mke na mume kwa zaidi ya miaka 36 na wamejaliwa kuwa na watoto wanne lakini mmoja Mungu alimpenda zaidi hivyo ni marehemu.

Aliendelea kusimulia kwa uchungu kwamba, mwaka 2000, aliugua ambapo mumewe Chidumule alimpeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili na kugundulika kuwa ana ugonjwa wa kisukari.

“Baadaye mume wangu alianza kuaga nyumbani kuwa anakwenda kwenye huduma, akawa anakaa huko wiki mbili bila kuniuliza naendeleaje na familia kabla ya kuamua kuondoka moja kwa moja.
“Ukweli ninateseka na sina msaada wowote kwani wanangu hawana kazi, ninatakiwa kwenda hospitali kila mara lakini wakati mwingine nakosa fedha.
 
Mkongwe wa Nyimbo za Injili Bongo, Rev. Cosmas Chidumule
 “Wakati mwingine tunakosa hata chakula kwa kuwa sina nguvu tena ya kufanya kazi. Naomba msaada kwa Watanzania wenzangu kwani nateseka sana. 

“Ni miezi mitatu sasa, Chidumule hajakanyaga hapa nyumbani (Kinondoni B) na aliondoka tangu tulipomaliza msiba wa mtoto wetu, amenishtaki Ustawi wa Jamii ambapo niliitwa lakini waligundua sina kosa ndipo akaambiwa kama vipi aende mahakamani hivyo ndiyo nasubiri kuitwa mahakamani (bila kutaja kosa),” alisemahuku akiangua kilio. 

Jitihada za kumpata Chidumule ziligonga mwamba kwani simu yake ya kiganjani haikuwa hewani muda wote hivyo jitihada zinaendelea. 
Kama umeguswa na habari hii na ungehitaji kumchangia mama huyu chochote ulichonacho, wasiliana naye kwa namba 0653 117535.

Comments