HAMIS Kiiza amefanya mazoezi na Wabrazili, Genilson Santos ‘Jaja’ na Andrey Coutinho kwa siku tatu tu, lakini akasema watakuwa bora zaidi endapo watafanya vizuri katika mechi za Uwanja wa Taifa na Mkwakwani, Tanga.
Kauli hiyo ya Kiiza imekuja baada ya juzi Jumanne kuchezeshwa nafasi ya mshambuliaji pacha na Jaja na kuonekana kuelewana kwa kiasi kikubwa na kuweka matumaini ya safu yao ya ushambuliaji kufanya vizuri msimu ujao.
Kiiza aliliambia Mwanaspoti: “Nimemuona Jaja ni mzuri na hata nilipocheza naye nimemuona anajua anachofanya, ataisaidia timu endapo kile anachofanya mazoezini kitafanyika pia katika mechi.
“Tatizo la mpira wa Tanzania anatakiwa acheze vizuri Uwanja wa Taifa na hata Mkwakwani maana huko watu hawana uvumilivu na wanaweza hata kuwapiga mawe kama hawatakomaa na kupambana uwanjani.”
Mshambuliaji huyo raia wa Uganda alisema hata yeye alipokuja Tanzania alipendwa na kila shabiki na mwanachama, lakini siku mambo yalipoenda vibaya alikosolewa hata kwa kurushiwa chupa.
“Hii ndiyo Yanga, lazima wakomae la sivyo watauona mpira wa Afrika mchungu, mimi nilipendwa hapa, lakini siku moja nikarushiwa hadi chupa za maji kwa mambo kutoenda vizuri uwanjani,” alisema Kiiza.
Comments
Post a Comment