COASTAL Union imeingia hasara kwani haitapata hata shilingi kutoka Simba baada ya beki wao Abdul Banda juzi Jumanne jioni kusaini mkataba wa miaka mitatu ya kuichezea Simba msimu ujao wa Ligi Kuu Bara unaotarajia kuanza Septemba 20 mwaka huu.
Awali Coastal Union iligoma kuwauzia Simba mchezaji huyo kwa madai kuwa bado wanamuhitaji hivyo wasingekuwa tayari kupokea kiasi chochote cha fedha kutoka Simba ili kumwachia, lakini kwa sasa imeambulia patupu baada ya kushindwa kuheshimu mkataba wa mchezaji huyo.
Banda alisaini mkataba huo baada ya uongozi wa klabu yake ya zamani kushindwa kumlipa mishahara yake ya miezi mitatu ambapo jumla ni Sh 900,000 kwani alikuwa akilipwa Sh 300,000 kwa mwezi, mishahara hiyo ni kuanzia Mei, Juni na Julai huku usajili wake Simba ikiwa ni Sh 20 milioni.
Beki huyo juzi Jumanne akiwa na Meneja wake Abdul Bosnia walitua jijini Dar es Salaam na kuwasilisha barua ya kuvunja mkataba na Coastal katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa madai ya kuwa wamekwenda kinyume na makubaliano ya mkataba wake na hivyo kuwa mchezaji huru.
Banda na Meneja wake waliondoka jana Jumatano asubuhi kurudi jijini Tanga ambapo leo Alhamis atawasili kujiunga na Wekundu hao wa Msimbazi na tayari uongozi wa Coastal kupitia Makamu Mwenyekiti, Steven Mnguto, amekabidhiwa barua hiyo ingawa yeye alikanusha.
“Banda ni mchezaji huru baada ya Coastal kushindwa kumlipa mishahara yake, tumekuja Dar es Salaam kuleta barua TFF na kwa bahati nzuri Mwenyekiti Mnguto naye tumempa, mishahara yake ataendelea kudai kwani wao ndiyo walienda kinyume na mkataba.
“Banda kwa sasa ni mchezaji wa Simba baada ya kumalizana kila kitu, atarudi Alhamisi (leo) kujiunga na timu yake mpya, mpira ni ajira yake inayomwendeshea maisha ya kila siku hivyo hawezi kuendelea kuishi maisha ya shida katika timu bila kulipwa mishahara wakati kuna timu zinamhitaji,” alisema Bosnia.
Banda ameliambia Mwanaspoti kuwa kikubwa anachokiomba kutoka Simba ni ushirikiano ili timu iweze kufanya vizuri msimu ujao.
“Huwa sichagui wapi nicheze, nacheza timu yoyote ili mradi maslahi ni mazuri, Coastal ni timu ambayo nimetoka nayo mbali lakini imeshindwa kunitimizia mahitaji yangu hasa mshahara ndio maana nimeamua kusaini Simba, yote ni kutafuta maisha,” alisema Banda.
Mmoja wa mabosi wa Simba aliliambia Mwanaspoti akisema: “Ni mchezaji huru hivyo hatuwezi kuilipa Coastal gharama za kuvunja mkataba wao ndio wamevunja, kushindwa kumlipa mishahara miezi mitatu ni kinyume na taratibu za mkataba, labda tuwaonee huruma tu, akirudi Dar es Salaam tutaenda kumkabidhi jezi yake.” Kwa upande wa Coastal, Steven Mnguto ambaye ni Makamu Mwenyekiti wao alisema: “Tunajua ni mchezaji wetu ingawa kweli hajalipwa mishahara yake hiyo na si yeye tu wachezaji wote hawajalipwa na ni kwa sababu klabu haina fedha, barua ya kuvunja mkataba sijaipata labda nikienda Tanga Alhamisi (leo) ndio nitakuwa na chochote cha kuzungumza zaidi.”
Banda yupo chini ya Mwanasheria anayesimamia mkataba wake. Katibu Mkuu wa TFF, Celestine Mwesigwa alisema: “Kuna taratibu za upokeaji wa barua ila bado haijafika kwangu ikifika itafanyiwa kazi kwani nilikuwa nje ya ofisi.”
Comments
Post a Comment