Washtakiwa watatu wanaokabiliwa na mashtaka ya mauaji dhidi ya mtoto Nasra Rashid Mvungi, wamelazimika kubadilishiwa hakimu baada ya hakimu wa awali, kupata dharura na kutokuwepo mahakamanani hapo.
Washtakiwa hao ambao kesi yao imekuwa ikifikishwa na kutajwa, mbele ya hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Morogoro, Mary Moyo, walilazimika kupandishwa kizimbani mbele ya hakimu Agripina Kimanze na kusomewa mashtaka yao, baada ya hakimu moyo kutokuwepo mahakamani, ambapo tofauti na nyakati zingine, shauri hilo lilichelewa kuanza.
Mwendesha mashtaka wa polisi Aminatha Mazengo, akisoma shitaka, aliiambia mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na kwamba jalada bado lipo kwa mwanasheria mkuu wa serikali, hivyo kuiomba mahakama kupanga tarehe nyingine ya kutajwa kwa kesi hiyo.
Mahakama iliridhia ombi hilo, na kupanga Agosti 20 mwaka huu, kufikishwa tena kwa kesi hiyo kwaajili ya kutajwa, kutokana na mahakama hiyo kukosa uwezo kisheria kusikiliza shitaka la mauaji na washtakiwa kurudishwa rumande kutokana na kesi hiyo kutokuwa na dhamana.
Kesi hiyo ya mauaji inawakabili washitakiwa watatu akiwemo baba mzazi wa mtoto Nasra, bw. Rashid Mvungi pamoja na waliokuwa walezi wake, Bi Mariam Said na mumewe Mtonga Omary, ambao awali walikuwa wakikabiliwa na shitaka la kula njama na kufanya vitendo vya ukatili dhidi ya mtoto Nasrah Mvungi kabla ya baadaye mashitaka yao kubadilishwa na kuwa ya mauaji baada ya mtoto huyo kufariki dunia.
Comments
Post a Comment