KAGAWA APONA KWENYE FAGIO LA LOUS VAAN GAAL


KOCHA Louis van Gaal amekaa kitako na mastaa wake saba na mwisho wa kikao hicho kilichofanyika kwenye uwanja wa mazoezi wa klabu ya Manchester United huko Carrington akawaambia sita kati yao wanaondoka.

Kwenye orodha hiyo ya mastaa yupo pia beki wa kulia, Mbrazili Rafael.

Van Gaal alikaa na mastaa hao kina Marouane Fellaini, Wilfried Zaha, Nani, Shinji Kagawa na straika kinda Will Keane walizungumza kwa saa kadhaa jioni siku ya Jumamosi iliyopita baada ya mazoezi huko Carrington na kuwaeleza kwamba kati yao ni Mjapani, Kagawa pekee ndiye anayemhitaji kwenye mipango yake.

Mastaa wengine Fellaini, Zaha, Nani na Keane waliambiwa kwamba klabu imefungua milango na kwamba itasikiliza ofa kutoka klabu yoyote inayoonyesha kuwahitaji nyota hao.

Marouane Fellaini atauzwa ikiwa ni mwaka mmoja tu tangu alipojiunga na timu hiyo kwa uhamisho wa Pauni 27 milioni akitokea Everton.

Rafael ni jina lililoshtua wengi kwa kuwamo kwenye orodha hiyo baada ya timu hiyo kwa sasa kusaka beki mwingine wa kulia, huku Kagawa akiambiwa kwamba atabaki Old Trafford, lakini atakuwa na shughuli ya kupigania namba dhidi ya Ander Herrera na Juan Mata.

Kiungo Mbrazili Anderson na straika Javier Hernandez hawa mapema tu walishafahamu kwamba Man United inakaribisha ofa kwa ajili yao na hivyo kuzifanya klabu za Southampton, Inter Milan, Tottenham, Atletico Madrid na Juventus kuingia vitani huku Napoli ikimfukuzia Fellaini.

Newcastle inamtaka Zaha, lakini Man United itasikiliza ofa ya maana kutoka Crystal Palace, West Ham na Nottingham Forest.

Comments