Ebola:Hatimaye KenyaAirways yasitisha safari za ndege.
Hatimaye shirika la ndege la Kenya Airways limesalimu amri na kukubali shinikizo la kusitisha safari za ndege kuelekea mataifa matatu yaliyoathirika pakubwa na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola.
Afisa mkuu mtendaji wa shirika hilo Titus Naikuni alisema kuwa baada ya kupata ushauri wa shirikisho la Afya duniani WHO na wizara ya afya nchini Kenya shirikisho hilo limeamua kusimamisha safari zote za ndege kuenda Liberia na Sierra Leone.
Marufuku hiyo itaanza kutekelezwa kuanzia jumanne ijayo tarehe 19th Agosti 2014.
Hata hivyo shirika hilo lilisema kuwa litaendelea na safari zake kuelekea Nigeria.
Kama hatua za dharura abiria wote ambao walikuwa wamenunua tiketi za kuenda mataifa hayo watarejeshwa pesa zao .
Afisa Mkuu Mtendaji wa KQ anasema ni jambo la dharura kukomesha safari za ndege
Marufuku hiyo haitaathiri raiya wakenya ambao wanarejea nyumbani wala madaktari ama watu wanaoshiriki juhudi za kusimamisha mlipuko huo wa ugonjwa.
Shirika la ndege la KQ lilikuwa limepuza shinikizo la kusafiri kuenda Magharibi mwa Afrika hatua ambayo ilikuwa imevutia wadau nchini Kenya kutishia kuishtaki mahakamani ilikuishurutisha kukomesha safari hizo kwa hofu kuwa huenda ikasababisha kuenea kwa ugonjwa huo nchini Kenya.
Shirikisho la Afya duniani WHO lilizua hofu nchini Kenya lilipoitaja kama moja ya mataifa yenye athari kubwa ya kuenezwa kwa Ebola.
Ebola:Hatimaye KenyaAirways yasitisha safari za ndege.
Uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta ni kitovu muhimu cha usafiri wa ndege katika kanda ya Afrika Mashariki na kati .
Uwanja huo hupokea takriban ndege 76 kila wiki kwenda na kutoka Magharibi mwa Afrika.
Mapema juma hili athari ya ugonjwa huo wa Ebola ulipelekea shirika la ndege la Korea kusimamisha safari zake za ndege kuingia Kenya kwa hofu ya maambukizi ya Ebola.
Hadi kufikia sasa hakuna mkenya yeyote aliyepatikana na ugonjwa huo wa Ebola.
Watu zaidi ya 1000 wameaga dunia kutokana na ugonjwa huo katika mataifa ya Sierra Leone Guinea Libera na Nigeria.CHANZO BBC SWAHILI
Comments
Post a Comment