ETO'O ALIVYOMDUWAZA BABA KWA KULIPWA DOLA 200 KWA WIKI


SUPASTAA, Samuel Eto’o, anafahamika bayana kuwa ni mmoja wa wanasoka makini zaidi duniani waliowahi kutokea kwenye Bara la Afrika.

Akitamba kwenye nafasi ya straika, Eto’o, aliliweka jina lake kwenye kumbukumbu za soka wakati alipokuwa akicheza Hispania kwenye michuano ya La Liga.

Bado anatambulika kuwa staa wa Cameroon mwenye hadhi kubwa zaidi, licha ya sasa kukosa timu ya kuichezea baada ya mkataba wake wa mwaka mmoja kufika ukingoni klabuni Chelsea. Hata hivyo, kuna mambo ambayo hayafahamiki kuhusu staa huyo wa zamani wa Barcelona.

Azaliwa na kukulia uswahilini Cameroon

Eto’o kwa sasa ni staa wa nguvu. Japo hakuzaliwa katika familia ya kimasikini, lakini mwanasoka huyo alikulia katika mazingira ya kawaida huko Cameroon.

Alizaliwa Machi 10, 1981 mjini huko Nkon, Cameroon. Eto’o ni mtoto wa baba mhasibu. Alianza kucheza soka katika academy ya Kadji Sports iliyopo huko Douala.

Apachikwa jina la Milla, akataliwa Ufaransa

Kutokana na kuonyesha kipaji cha soka tangu akiwa mdogo, Eto’o alipachikwa jina la utani la “Little Milla” ikiwa na maana ya mwanasoka mashuhuri zaidi Cameroon, Roger Milla.

Uhusiano wake wa Milla ulikuwa mkubwa zaidi baada ya kipindi hicho cha utotoni alipopenyapenya kwenye kundi la watu na kwenda kuchukua jezi ya staa huyo wa Cameroon kwa kipindi hicho.

Kipaji chake cha mpira kikamfanya aenda Ufaransa mahali ambapo alikataliwa kutokana kuwa mdogo na hakuwa na utambulisho unaokidhi matakwa yao.

Kama bahati kwake, akanaswa na academy ya klabu ya Real Madrid mwaka 1997, huku akiwa hana rekodi ya kuichezea timu hiyo. Alitolewa kwa mkopo mara kadhaa katika miaka hiyo ya tisini.
 Apeleka nyumbani Dola 200 kila wiki

Mara ya kwanza baada ya kuanza kulipwa kutokana na soka lake, Eto’o,  alikuwa akilipwa zaidi ya Dola 200 kwa wiki.

Familia yake iliona pesa hizo ni nyingi sana na hawakuamini kama mtoto wao angeweza kulipwa kiasi hicho kutokana na kucheza mpira.

Siku moja kwenye mahojiano, Eto’o, alijaribu kukumbushia alichoambiwa na baba yake, alisema: “Hivi unaweza kupata pesa zote hizi kwa ajili ya kucheza mpira tu?”

Jambo hilo lilimtia nguvu Eto’o na kucheza kwa nguvu zaidi ili kupata pesa nyingi zaidi tofauti na mwanzoni. Hadi anaondoka Chelsea, Eto’o alikuwa akilipwa zaidi ya Pauni 100,000 kwa wiki.

 Apata hati ya kusafiria ya Hispania, lakini abaguliwa

Baada ya kuishi Hispania kwa karibu muongo mmoja aking’ara kwenye La Liga, hilo lilimfanya Eto’o kufuzu vigezo vya kukabidhiwa hadi ya kusafiria ya Hispania.

Kutokana na hati hiyo, Eto’o, hakuhesabika tena kama mchezaji wa kigeni kwa nchi ya Hispania. Lakini, hilo halikumfanya asibaguliwe.

Mwaka 2005, kwenye mechi ya Real Zaragoza, mashabiki wa timu pinzani walikuwa wakiigiza milio ya nyani kila Eto’o alipogusa mpira jambo hilo lilisababisha mashabiki wawili kufungiwa miezi mitano kutojihusisha na mambo ya michezo.

Eto’o hakuona kama adhabu hiyo inatosha na alitaka Zaragoza icheze bila ya mashabiki na kutokana na hilo staa huyo wa Cameroon aliacha kwenda na familia yake kwenye mechi.
Akutana na mrembo Georgette, ambeba jumla

Kwenye pilikapilika zake, Eto’o alikutana na mrembo Georgette na Juni 2007 alimbeba jumla mchumba wake huyo ambaye alidumu naye kwenye mapenzi kwa kipindi kirefu kidogo.

Muda mwingi Eto’o na mkewe wamekuwa wakiutumia kwenye jiji la raha huko Paris, Ufaransa na walifanya hivyo kila walipopata nafasi ya kwenda kula maisha na familia yake yenye watoto watatu; Etienne, Maelle na Siena.

Aweka rekodi Hispania na Afrika

Eto’o ameweka rekodi kadhaa nchini Hispania akiwa mchezaji wa Kiafrika aliyecheza mechi nyingi.

Staa huyo alidumu kwa miaka kadhaa kwenye kikosi cha Real Madrid kabla ya kutolewa kwa mkopo Leganes na Espanyol. Kisha akacheza kwa misimu minne katika klabu ya Mallorca kabla ya kucheza misimu mitano Barcelona.

Kwa kipindi chake alichochezea Barcelona, Eto’o alifunga mabao 108 katika mechi 108. Kwa upande wa Afrika, Eto’o amekuwa na rekodi za aina yake na akiwa mchezaji aliyetwaa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Afrika mara nne; mwaka 2003, 2004, 2005 na 2010. Alishika nafasi ya tatu kwenye tuzo ya Fifa ya Mwanasoka Bora wa Dunia mwaka 2005.

Kuna watu waliibua mjadala kwamba aligomewa nafasi ya kwanza kwa kuwa ni Mwafrika. Ana miliki medali ya dhahabu pia ya michezo ya Olimpiki, medali mbili za ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika na ndiye kinara wa mabao wa nyakati zote nchini Cameroon na anashika namba tatu kwa kucheza mechi nyingi katika kikosi cha Simba Wasioshindika.

 Awatukana Real Madrid, Warusi wamjaza pesa
Eto’o alijikuta kwenye wakati mgumu kwenye msimu wa 2004-2005 wakati Barcelona iliponyakua ubingwa wa La Liga. Barca iliandaa sherehe Nou Camp kujipongeza kwa ubingwa, kwenye sherehe hiyo Eto’o alisikika akipiga kelele kutamka maneno: “Madrid, carbon, Saluda al campeón” (akiwa na maana “Madrid, wapumbavu, piga saluti kwa mabingwa.”)

Jambo hilo lilimfanya alazimike kuomba radhi hadharani kwa sababu Real Madrid ndiyo iliyokuwa klabu yake ya kwanza kwenye soka la kulipwa.

Baada ya mambo hayo kupita ilipofika mwaka 2011, klabu ya Anzhi Makhachkala ya Urusi ilimsajili Eto’o na kumfanya kuwa mchezaji anayelipwa pesa nyingi zaidi duniani kwa upande wa mishahara. Alikuwa akipokea Dola 26.8 milioni kwa mwaka na hapo akawapiku mastaa wote wa soka akiwamo Cristiano Ronaldo na Lionel Messi.

Kichaa wa magari, apambana kukuza soka Afrika

Eto’o ameandika vitabu tisa vya picha akizungumzia historia ya maisha yake. Ametumia lugha ya picha ili kuwarahisishia watoto wanaopenda kusoma historia yake.

Ukiliweka hilo kando, Eto’o ni kichaa wa magari ya kifahari. Akiwa na kipato cha Dola 75 milioni, hakutaka kuziacha pesa hizo zibaki tu kwenye akaunti yake ya benki na hivyo akawekeza katika kununua magari ya kifahari. Ana magari mengi ikiwamo Bugatti Veyron, Aston Martin One-77, na Maybach Xenatec.

Staa huyo pia hajasahau kusaidia jamii yake nchini Cameroon. Eto’o anamiliki mradi wake binafsi (Fundación Privada Samuel Eto’o) ambao umewekeza zaidi katika kukuza soka kuanzia kwenye shule za msingi. Eto’o amejenga pia shule za soka katika nchi za Gabon na Nairobi, Kenya.

 Umri wake wazua mjadala Chelsea

Mrembo wa Kitaliano msusi wa nywele, Anna Barranca, mpenzi wa zamani wa Eto’o na mama wa mtoto wa staa huyo, miezi michache iliyopita aliibuka na kudai kwamba Eto’o anaficha ukweli kuhusu umri wake.

Jambo hilo liliibuka baada ya kocha wa Chelsea, Jose Mourinho, kutia shaka kuhusu umri wa mchezaji huyo kitu ambacho Anna aliunga mkono na kudai mchezaji huyo ana umri mkubwa kuliko anaoutaja au kuandika katika wasifu wake.

Mourinho alisema: “Ninaye Eto’o, lakini ana umri wa  miaka 32, pengine inaweza kuwa 35, nani anajua?”.

Anna Barranca alidai kwamba umri wa mchezaji huyo ni mkubwa zaidi na kwamba alikuwa na miaka 39.


Comments