Benki ya NBC tawi la Moshi.
Katika hukumu hiyo iliyotolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kilimanjaro, Simon Kobelo, askofu huyo amehukumiwa kifungo hicho pamoja na raia watano wa Kenya baada ya kupatikana na hatia ya kufanya wizi huo kwa mtutu wa bunduki.
Moshi. Askofu wa Kanisa la Christian Fellowship Assemblies of God la Arusha, Jumanne Kilongola amehukumiwa kifungo cha miaka 32 jela baada ya kupatikana na hatia ya kupora Sh5.3 bilioni ndani ya Benki ya NBC, Tawi la Moshi Mei 21, 2004.
Katika hukumu hiyo iliyotolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kilimanjaro, Simon Kobelo, askofu huyo amehukumiwa kifungo hicho pamoja na raia watano wa Kenya baada ya kupatikana na hatia ya kufanya wizi huo kwa mtutu wa bunduki.
Kati ya fedha hizo, Sh126.2 milioni zilikuwa mali ya Benki ya NBC wakati Sh5.1 bilioni ni mali ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambayo ilikuwa ikitumia NBC Moshi kama kituo chake kidogo.
Ilielezwa mahakamani hapo wakati wa ushahidi kuwa Askofu Kilongola ndiye aliyekodi gari aina ya Toyota Landcruiser lililotumiwa kubeba fedha hizo kwa Sh320,000 na alimweleza mmiliki wake kuwa alikuwa anakwenda kubeba wanakwaya wake.
Raia wa Kenya waliohukumiwa kifungo hicho cha miaka 32 ni Wilfred Onyango Nganyi, Patrick Muthee Murithi, Gabriel Kungu Kariuki, Jimmy Maina Njoroge na Simon Ndungu Kiambuthi.
Hata hivyo, mahakama hiyo iliwaachia huru raia wengine watatu wa Kenya, Boniface Mwangi Mburu, David Ngugi Mburu na Michael Mbanya Wathigo kutokana na kukosekana ushahidi dhidi yao.
Hakimu Kobelo alisema upande wa mashtaka ukiongozwa na mawakili wa Serikali, Hyra Sande, Ladslaus Komanya na Stella Majaliwa umethibitisha pasipo shaka kuwa washtakiwa hao waliohukumiwa walitenda makosa hayo.
Alisema ushahidi dhidi ya Askofu Kilongola na raia hao wa Kenya ulikuwa madhubuti kutokana na kutambuliwa kikamilifu na mashahidi katika gwaride la utambuzi.
Hakimu huyo alisema Mahakama imewahukumu kifungo cha miaka 30 kwa unyang’anyi wa kutumia silaha na miaka mingine miwili kwa kosa la kula njama ya kupora fedha hizo.
Hakimu Kobelo aliamuru Dola za Marekani 39,000, sawa na Sh64 milioni walizokutwa nazo washtakiwa zitaifishwe na Serikali na zikabidhiwe kwa uongozi wa Benki ya NBC. Hukumu hiyo imekuja wakati jitihada za Tanzania kuwarejesha nchini, wahalifu watatu kutoka Kenya na Uganda, wanaodaiwa kuvamia benki hiyo zikiwa zimegonga mwamba.
Watuhumiwa hao ni Patrick Ayis Ingoi, raia wa Kenya anayedaiwa kuwa kiongozi wa genge la majambazi hao, Charles Lumago na Shaban Wayabona ambao ni raia wa Uganda.
Hukumu hiyo inafanya idadi ya waliofungwa kwa uporaji huo kufikia 12, baada ya Watanzania wanne kufungwa kwa kosa hilohilo Desemba 13, mwaka 2006.
chanzo; mwananchi.
Comments
Post a Comment