Bomu la kujitoa muhanga lalenga kanisa Jumapili ya matawi, waumini wajeruhiwa

 

Shambulio linaloshukiwa kuwa la bomu la kujitoa muhanga nje ya kanisa Katoliki katika mji wa Makassar nchini Indonesia limejeruhi takribani watu 14 , polisi wanasema.

Polisi wamesema mlipuko ulitokea wakati washambuliaji wawili walipojaribu kuingia kanisani Jumapili ya matawi, siku ya kwanza ya Pasaka.

Pikipiki iliyoharibiwa na sehemu za mwili zilipatikana katika eneo la tukio na polisi walisema washambuliaji hao wawili walikuwa wamekufa.

Wanamgambo wa Kiislamu walishambulia makanisa hapo zamani lakini hakuna kundi ambalo lilikiri kutekeleza mashambulizi hayo.

Rais wa Indonesia Joko Widodo alilaani shambulio hilo kama "kitendo cha ugaidi" na akasema alikuwa amemwagiza mkuu wa polisi kuchunguza waliohusika.

"Natoa wito kwa kila mtu kupigana dhidi ya ugaidi na msimamo mkali, ambao ni kinyume na maadili ya kidini," rais alisema.


Waziri wa Masuala ya Kidini Yaqut Cholil Qoumas aliwasihi polisi kuongeza hatua za usalama katika sehemu za ibada.

Wakati wa misa ya Jumapili ya mitende huko Vatican, Papa Francis aliwaombea waathiriwa wa shambulio hilo.

Tunafahamu nini kuhusu shambulio hilo?

Mlipuko ulitokea majira ya saa nne na nusu saa za eneo hilo mwishoni mwa ibada ya Jumapili ya matawi.

''Kulikuwa na watu wawili wakiendesha pikipiki wakati mlipuko ulipotokea katika lango kuu la kuingilia katika eneo la kanisa- watu hao walikuwa wakijaribu kuingia katika uwanja wa kanisa, '' msemaji wa polisi Argo Yuwono alisema.

Kisha baadae, Mkuu wa usalama nchini humo, Mahfud MD, aliliezea tukio hilo kuwa ''bomu la kujitoa muhanga'' lililotekelezzwa na watu wawili, ambao wote walikufa.

Sehemu za miili zilitapakaa barabarani

Padre katika kanisa hilo, Wilhemus Tulak, aliiambia Televisheni ya Metro TV kuwa walinzi walikuwa wamekabiliana na mtu mmoja anayeshukiwa kuwa mshambuliaji.

Mshambuliaji huyo, alisema, alifika kwa pikipiki na kujaribu kuingia kanisani.

Polisi walisema watu wasiopungua 14 walijeruhiwa, pamoja na maafisa wa kanisa ambao waliwazuia washambuliaji kuingia katika kanisa kuu.



Comments