Uchaguzi wa Tanzania 2020: Je upi msingi wa madai kuwa rais wa Zanzibar huamuliwa Dodoma?

Magufuli na Dkt Shein
'Dodoma' imekuwa ikitoa maamuzi ya kushtukiza, hata rais John Magufuli na Dkt Shein hawakupigiwa chapuo walipojitosa kugombea urais wa Tanzania na Zanzibar mtawalia.

Katika mchakato wa kutafuta mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000, Amani Karume, aliyekuja kuwa mgombea wa chama hicho na baadaye Rais wa Zanzibar, hakuwa mgombea aliyeungwa mkono na wengi visiwani humo.

Kulikuwa na kundi kubwa zaidi lililokuwa likimuunga mkono Dk. Mohamed Ghalib Bilal -aliyekuwa Waziri Kiongozi wakati wa utawala wa Dk. Salmin Amour na akidaiwa kuungwa mkono na bosi wake wa zamani.

Inafahamika kwamba Salmin alikuwa nampango wa kutaka kuongezewa kipindi kingine cha kuongoza kama Rais kinyume cha matakwa ya kikatiba. Baada ya juhudi zake hizo kupingwa hadharani, wafuasi wake walihamia kwa Bilal.

Taarifa zilizotoka Zanzibar wakati ule zilieleza kwamba katika wagombea waliojitokeza, Karume alishika namba nne katika mpangilio wa wagombea walioonekana kufaa zaidi kuongoza visiwa hivyo baada ya Salmin.

Hata hivyo, wakati wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM walipopiga kura mjini Dodoma, Karume alipata kura 111 dhidi ya kura 67 alizopata Bilal. Akatangazwa kuwa mgombea.
Kikao cha mchujo wa awali Wa wagombea kilifanyika Zanzibar wiki ilopita chini ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Dkt Ali Mohammed Shein.
Kikao cha mchujo wa awali wa wagombea kilifanyika Zanzibar wiki ilopita chini ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Dkt Ali Mohammed Shein(Kulia)

Ndipo dhana kwamba mgombea urais wa CCM Zanzibar huwa hatafutwi visiwani humo isipokuwa hupangwa na kupigiwa kura na wajumbe wa chama hicho ambao hufanyia mikutano yao katika Makao Makuu ya nchi - Dodoma.

Lakini, je ni kweli kwamba Rais wa Zanzibar huamuliwa Dodoma na kwamba kinachotokea huwa hakina maslahi na visiwa hivyo isipokuwa maslahi ya Tanzania Bara?

Dodoma kama 'machinjio' ya wagombea

Kuelewa dhana hii, ni muhimu sana kuelewa siasa za Zanzibar na kwa hakika kuelewa siasa za nchi nyingi za Afrika ambazo ni visiwa.

Kwa kawaida, kihistoria tangu nyakati za kutafuta Uhuru (Mapinduzi) hadi sasa, Wazanzibari si watu ambao huwa wanakubaliana moja kwa moja kwenye kila kitu.

Tuchukulie mfano wa tukio muhimu zaidi la kisiasa Zanzibar katika kipindi cha miongo sita iliyopita - Mapinduzi ya mwaka 1964. Hadi leo, ukizungumza na Wazanzibari, kuna mgawanyiko kuhusu nini hasa kilitokea na taathira yake.

Ukimsikiliza Maalim Seif Shariff Hamad; mmoja wa wanasiasa wakongwe visiwani humo na ukimsikiliza Ali Karume ambaye ni mtoto wa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Karume utapata picha tofauti kuhusu mapinduzi haya kuanzia malengo yake na taathira zake.

Wazanzibari wengi wana tafsiri zinazokinzana kuhusu jambo hili moja la Mapinduzi.
Angalia suala hilo la Dk. Salmin Amour kutaka kuongeza kipindi kingine cha kutawala. Kwa upande mmoja; humohumo ndani ya CCM Zanzibar kuna waliokuwa wakiunga mkono nakuna waliokuwa hawaungi mkono.

Wakati ule, mwaka 2000, wanasiasa wawili walikuwa mfano tosha wa mgawanyiko huu. Ali Ameir Mohamed alikuwa akitajwa kama mtu aliyeunga mkono jambo hilo huku nyota mwingine wa siasa za Zanzibar wakati ule, Mohamed Seif Khatib, akipinga jambo hilo.

Kuna suala lingine zito la 'kuchafuka' kwa hali ya hewa visiwani Zanzibar kulikosababisha kujiuzulu kwa Aboud Jumbe ndani ya CCM na serikalini.

Huyu alikuwa Rais wa Zanzibar ambaye alilazimishwa kuachia wadhifa wake huo na nyingine zote za kwenye chama kwenye kikao kilichofanyikia - Dodoma.
Dkt. Hussein Mwinyi
Dkt. Hussein Mwinyi anapigiwa chapuo zaidi kunyakua tiketi ya kugombea urais Zanzibar, japo lolote laweza kutokea Dodoma.

Lakini, hadi leo, inajulikana kwamba wapo wanachama ndani ya CCM Zanzibar ambao hawakuunga mkono mambo yaliyokuwa yakifanywa na Jumbe kiasi kwamba ndiyo walioviarifu vyombo vya dola kuhusu kinachoendelea.

Kwa hiyo, hata jambo hilo la Jumbe ambalo nalo limekuwa likisemwa kama ni ushahidi wa kuonyesha namna 'Dodoma' inavyofinya maslahi ya wagombea; halikuwa jambo lililoungwa mkono na Wazanzibari wote.

Kwa hiyo, tatizo kubwa la Zanzibar si Dodoma bali ni mgawanyiko wa kisiasa ambao hutokea kwa karibu kila jambo kubwa linalotokea.

Hata mwaka 2000 wakati Amani Karume anamzidi Bilal, kulikuwa na mvutano wa makundi ya vijana na wazee; Karume akivutia damu changa kwenye chama na Bilal akiwa kipenzi cha wale wakongwe.

Dodoma na CCM Bara

Kama Edward Lowassa angekuwa Mzanzibari, ni wazi kwamba leo kitendo cha jina lake kukatwa Dodoma kingeweza kuchukuliwa kuwa ni ushahidi mmoja wapo kwamba mji huo haujali maslahi mapana ya kisiasa ya Zanzibar.

Lakini Lowassa ambaye alikuwa kipenzi cha wajumbe wa vikao vya juu vya CCM hakupitishwa na chama hicho kuwa mgombea wake wa Urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Mwanasiasa huyo baadaye alihamia upinzani na kugombea urais Oktoba 2015 na kushindwa na rais wa sasa John Magufuli. Lowassa hatimaye alirejea CCM mwaka 2019.

Lowassa
Edward Lowassa alirejea CCM mwaka 2019.

Mwanasiasa mwingine ambaye anaweza kulalamika pia kuhusu Dodoma ni John Samuel Malecela; aliyepata kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania na mwanasiasa ambaye kuna kipindi alipewa jina la tingatinga la kisiasa kutokana na umahiri wake wa kufanya shughuli za kisiasa.

Kati ya mwaka 1995 hadi 2005, Malecela - ambaye ni mzaliwa wa Dodoma, alinyimwa fursa mbalimbali za kuwania nafasi nyeti za uongozi kwa uamuzi uliokuwa ukichukuliwa kupitia vikao vya CCM vilivyofanyikia Dodoma.

Katika mahojiano na mwandishi wa makala hii, mtoto wa Malecela, Mwele, alieleza kwamba baba yake aliumizwa na matukio hayo lakini imani yake kubwa kwa chama ndiyo iliyomfanya abaki pasipo kuhama.

Malecela hakuwahi kulalamika hadharani kuhusu alichofanyiwa na chama chake wala 'roho mbaya' ya maamuzi ya Dodoma.

Je, nini hutokea Dodoma?

Ingawa Lowassa alionekana kuwa mwanasiasa aliye kipenzi cha wana CCM wengi mwaka 2015, vyombo vya kichunguzi vya chama hicho vilishauri chama kwamba mgombea ambaye angekipa ushindi wa uhakika ni mmoja tu; John Magufuli.

Katika uhai wake, chama hicho kimekuwa nautaratibu wa kufanya uchunguzi kuhusu watu wanaotafuta nafasi za juu za uongozi na mwishowe mtu anayeonekana na sifa za kushinda uchaguzi, ndiye ambaye hatimaye hupewa nafasi hiyo.

Kwa hiyo, vikao vya mwisho vya Dodoma huwa ni hitimisho tu la safari ndefu ambayo chama hukipitia katika kumtafuta mgombea anayefaa na atakayekiuza chama hicho.

Katika kueleza hili, Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Pius Msekwa, alipata kusema kwamba kazi ya kwanza na muhimu kulizo zote ya chama cha siasa ni kushinda uchaguzi. Huyu ni mtu ambaye alikuwa Katibu Mtendaji wa kwanza wa CCM.

Kinyang'anyiro cha Zanzibar 2020

Ingawa CCM haijatangaza rasmi majina matano yatakayopelekwa Dodoma kwa ajili ya uamuzi wa vikao vya juu vya chama hicho; inaaminika kwamba makada watano; Dkt. Hussein Mwinyi, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa, Dkt. Khalid Salum Mohamed, Shamsi Vuai Nahodha na Hamisi Mussa ndiyo waliopewa alama za juu na vikao vya Zanzibar.

Uchaguzi wa mwaka huu umezua mjadala kutokana na idadi kubwa ya wagombea walioonyesha nia ya kutaka kurithi nafasi ya Dkt. Ali Mohamed Shein. Wagombea 32 walijitokeza; rekodi katika siasa za Zanzibar.

Mshindi katika mchakato huu wa ndani ya CCM ndiye antarajiwa kushindana na mgombea wa Chama cha ACT Wazalendo, Seif Shariff Hamad, anayetarajiwa kupitishwa na chama chake kuwania nafasi hiyo.
Maalim Seif
Pamoja na idadi hiyo kubwa, viongozi wa chama hicho hawakupata taabu kuchagua waliofaa. Taarifa kutoka ndani ya vikao vya Zanzibar ziimeonyesha kwamba kuna wajumbe ambao hawakuwa na nia hasa ya kutaka Urais lakini walitaka tu kutumia nafasi hiyo kujitangaza.

Wagombea hawa watano wana sifa na uzoefu tofauti katika siasa za Zanzibar; Mwinyi -mtoto wa Rais wa pili wa Tanzania; ni mwanasiasa mwenye uzoefu wa miaka takribani 20 kama mbunge na waziri katika Serikali ya Tanzania.

Profesa Mbarawa ni msomi aliyewahi kufanya kazi ndani na nje ya nchi kwa muda mrefu na amekuwa waziri kwenye serikali ya Rais Jakaya Kikwete na ya sasa ya Rais Magufuli.

Shamsi amewahi kuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar kwa muda wa miaka kumi na amepata kuwa waziri wa wizara tofauti katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Khalid ni mchumi aliyewahi kuwa Waziri wa Fedha na Katibu Mkuu wa wizara hiyo na ni miongoni mwa wanasiasa wanaoelezwa kuwa na ubongo unaochemka katika masuala ya uchumi.

Mussa amekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi kwa takribani miaka 16; akianza wakati wa urais wa Amani Karume na kuendelea na Dk. Shein. Anatajwa kama mmoja wa wachumi mahiri wa Zanzibar.

Hata hivyo, Dk. Mwinyi anatajwa kuwa mgombea anayekubalika zaidi miongoni mwa watano hao. Ndiye mgombea anayejulikana zaidi, mwenye mtandao mkubwa zaidi marafiki, asiye na kashfa ya kisiasa na anayeonekana amejiandaa muda mrefu kwa nafasi hiyo.

Amekuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM; chombo cha juu zaidi cha maamuzi cha chama hicho kwa muda wa miaka kumi na hivyo anajuana na wapiga kura wengi kuliko wenzake.

Shamsi anaonekana kuwa amepita katika siku zake bora- huku Khalid na Mussa wakiwa na jambo la kutojulikana sana na wajumbe wa Tanzania Bara kutokana na kufanya kazi zao Zanzibar kwa muda mrefu.

Hata hivyo, hiyo inategemea pia 'Dodoma' itakuwa na taarifa zipi za ziada dhidi ya wagombea hao watano.

Pasi na shaka yoyote; nikimnukuu Pius Msekwa, taarifa ya muhimu zaidi ikiwa; Ni nani atakipa ushindi chama hicho kwenye mchuano dhidi ya Seif Shariff Hamad.

Comments