Ndalichako azindua Chuo kipya cha VETA “mkimaliza hapa ajira nje nje”



Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amezindua Chuo cha Ufundi Stadi Nyamidaho kilichopo Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma.

Akizungumza katika hafla hiyo ya uzinduzi, Profesa Ndalichako amesema uanzishwaji wa Chuo hicho ni mwendelezo wa utekelezaji wa azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga vyuo vya ufundi stadi katika kila Wilaya Nchini ili kupeleka huduma hiyo karibu na Wananchi na kuwapatia ujuzi vijana wa kitanzania.

Ndalichako amesema Chuo cha Nyamidaho kimetokana na majengo yaliyokuwa yakitumiwa na Taasisi ya World Vision ambapo Serikali imekarabati majengo yaliyokuwepo na kujenga mengine mapya.

Waziri Ndalichako ameeleza kuwa jumla ya Shilingi milioni 534 zilitolewa kwa ajili ya kazi hiyo na kwamba zimetumika milioni 477 hadi ukamilishaji. Aidha ameridhia ombi la kiasi kilichobaki kutumika kuanzisha ujenzi wa bweni la wanafunzi wa kiume.

Ameongeza kuwa katika Mwaka 2019/20 vyuo 10 vya Halmashauri za Wilaya vimejengwa na kuanza kutoa mafunzo.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Emmanuel Maganga ameishukuru Wizara ya Elimu kwa kukamilisha ujenzi wa chuo hicho na amewataka wakazi wa kijiji cha Nyamidaho kuhakikisha vijana wao hasa wa kike wanajiunga na chuo hicho.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya VETA, Peter Maduki ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuimarisha Elimu ya Ufundi nchini na kuongeza kuwa Chuo hicho kipya kina wanafunzi takriban 70. Aidha ameagiza Uongozi wa VETA kutoa bure mafunzo ya kozi ya uwashi kwa wanafunzi wanaotoka Nyamidaho.

NDALICHAKO AZINDUA VETA NYAMIDAHO KIGOMA | Full Shangwe Blog
Waziri Ndalichako amesema hayo wakati akizindua Chuo cha VETA, katika Kijiji cha Nyamidaho, Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma, ambapo amesema katika mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali inaendelea na ujenzi wa Vyuo vya Ufundi Stadi katika Mikoa ya Rukwa, Njombe, Kagera na Geita, kwa gharama ya Shilingi Bilioni 29.8.

Comments